Siamini katika kushindwa: Waziri Bashungwa

12Jun 2019
Augusta Njoji
DODOMA
Nipashe
Siamini katika kushindwa: Waziri Bashungwa

WAZIRI wa Viwanda na Biashara, Innocent Bashungwa amewaeleza watumishi wa wizara hiyo kuwa haamini katika kushindwa na kuwataka kuhakikisha hawamuangushi Rais John Magufuli na watanzania kwenye kufikia uchumi wa kati.

WAZIRI wa Viwanda na Biashara, Innocent Bashungwa akikabidhiwa ofisi na aliyekuwa Waziri wa wizara hiyo Joseph Kakunda.

Bashungwa ametoa kauli hiyo leo jijini Dodoma katika makabidhiano yake na aliyekuwa Waziri wa wizara hiyo Joseph Kakunda ambaye Rais John Magufuli alitengua uteuzi wake Juni 8, mwaka huu.

Amewataka watumishi kutumia changamoto zilizopo kama fursa kwao ya kuzifanyia kazi na kukidhi matarajio ya watanzania.

“Hii ndio Wizara ya kuwapeleka watanzania kwenye kipato cha kati, Hili ni deni kubwa kwa Rais na watanzania, naomba tufanye kazi kama ‘Team work’ kwa kuwa ndio ufunguo wa mafanikio,”amesema.

Ameongeza kuwa “Mimi falsafa yangu huwa siamini katika kushindwa naamini mkiamini kama mimi hakuna kinachofeli,”.

Bashungwa amesema pia atahakikisha anashirikiana na idara za masoko na biashara kwenye wizara ya viwanda na ile ya kilimo ili kuwapatia masoko ya uhakika wakulima.

“Kila misimu kuna kilio cha wakulima kuhusu masoko sasa idara hizi mbili zishirikiane kutafuta masoko ya wakulima nimeona kabisa hakuna ushirikiano mzuri wa hizi idara za masoko za wizara hizi mbili,” amefafanua.

Amewataka watumishi kutekeleza mpango mkakati uliopo ili kuleta matokeo chanya kwa vitendo.

Kwa upande wake, Kakunda ambaye ni Mbunge wa Sikonge amesema Wizara hiyo ndio inabeba maendeleo ya nchi hivi sasa hivyo umuhimu wake kila mtu anailaumu na kuisifu.

“Hii ni dhamana kubwa na jukumu kubwa limekasimiwa kwako na Rais, umetoa ahadi hutamuangusha isimamie hiyo ahadi, wafanyakazi msijisahau nyie mnaandika historia ya nchi hii, jitahidini kumsaidia Waziri ili kutimiza matarajio ya Rais na watanzania,”amesema.

Habari Kubwa