Sifa 10 za kiongozi mzuri ndani ya taasisi

01Sep 2018
Kelvin Mwita
DAR ES SALAAM
Nipashe
Sifa 10 za kiongozi mzuri ndani ya taasisi

WATU wengi wana shauku kubwa ya kuwa viongozi katika ngazi mbalimbali kwenye taasisi wanazofanyia kazi kwa malengo tofauti.

Wako wenye maono ya kuleta mabadiliko kwa kuwa hawaridhishwi na hali wanayoiona lakini wako ambao kiasili wanapenda tu uongozi, hivyo maisha yao yamekuwa  kutafuta fursa za uongozi.

 Kuna kundi lingine ambalo nia yao ya kutafuta madaraka au uongozi imeambatana na nia ovu yenye lengo la visasi na kuonea wengine.

Hata hivyo, sehemu yoyote viongozi hubaki kuwa kundi dogo zaidi ya lile la watu wanaoongozwa lakini kuna mazingira ambayo wanaotaka kuwa viongozi ni wengi kuliko wale wanaotamani kuongozwa.

Hii ni sababu tosha ya kumfanya mtu ajitofautishe na wengine kwa namna ya kipekee kabisa kwani uongozi ni sayansi na sanaa na mahali popote kuna kanuni na miiko yake.

Je, unatamani kuwa kiongozi mzuri? Fanya haya;

JIFUNZE KUJIONGOZA KWANZA

Watu wengi hutamani kuwa viongozi katika taasisi zenye watu wengi na wa kila aina lakini wao wenyewe wameshindwa kujiongoza.

Kiongozi mzuri ni yule ambaye amefanikiwa kujiongoza kwanza. Uwezo wako utaanza kupimwa kwa uamuzi ambao umeshawahi kuuchukua juu ya maisha yako na mtindo wa maisha unaoutumia.

Ni vyema kujifunza kujiongoza vyema kwanza. Maisha yako yanatakiwa yawe ushuhuda tosha wa kuwaaminisha wengine kwamba wakikupa dhamana ya uongozi utaweza kuyafanikisha malengo ya taasisi kwa ujumla.

AMINI UONGOZI NI DHAMANA

Moja ya vitu vinavyoziponza taasisi nyingi ni kuwa na viongozi wenye mawazo kuwa uongozi ni kwa ajili yao na si kwa maslahi mapana ya taasisi. Wengine pia huamini kuwa ukishakuwa kiongozi pengine wewe ni kiongozi wa milele.

Ni vyema kuanza kujitayarisha mapema kisaikolojia kwa kuamini kuwa uongozi pia ni dhamana ya muda mfupi ya kuwatumikia wengine kwa maslahi yao na si maslahi yako binafsi. Hii itakufundisha unyenyekevu, utii na kuwa mtumishi wa wengine na si ‘mungu mtu’. Ukishindwa katika hili utapata taabu sana wakati wa uongozi na baada ya uongozi kukoma.

ZIKUBALI TOFAUTI MIONGONI MWA WATU

Tumeumbwa tofauti tukiwa na vipawa na haiba tofauti lakini pia mazingira tuliyokulia na jitihada mbalimbali zimefanya binadamu tuwe tofauti katika mambo mengi. Kwa kiongozi ni vyema kuzikubali na kuzielewa tofauti mbalimbali na kuweka utu mbele.

Matendo na maoni yako yanatakiwa yasiwe ya kibaguzi wala ya dharau juu ya wanaume na wanawake, walio nacho na wasio nacho, wenye vyeo na wasio na vyeo, wa kabila hili na lingine, wa rangi hii na rangi ile na mambo mengine mengi.

Usiwaone wala usijione ni bora au upo kwenye kundi bora kuliko wengine na hii itatathminiwa na matendo na maneno yako kabla na wakati wa uongozi wako.

JIFUNZE KUJIFUNZA

Uongozi unahitaji ujuzi, uwezo na uzoefu tofauti tofauti, hivyo anza kuondoa fikra kuwa una sifa zote za uongozi.

Tumia fursa mbalimbali za kujiendeleza na kujiongezea maarifa kupitia kusoma vitabu na vyanzo vingine vya taarifa na pia kujifunza kwa watu wenye uzoefu na uwezo katika eneo hili. Ushawishi pekee haukupi sifa ya moja kwa moja kuwa kiongozi mzuri.

KUBALI KUKOSOLEWA

Ukiona unaamini kuwa wewe ni mkamilifu na chochote unachowaza, kuamini, kusema na kufanya ndicho sahihi, anza kubadilisha huu mtazamo.

Kwa kuamini kuwa kila mtu ana upungufu wake inatosha kabisa kuwa na sababu ya kubadili mtazamo huu.

Jenga mazingira ya kukoselewa na kupokea maoni kwa waliokuzidi na uliowazidi. Kiongozi mzuri ni msikivu na hili halimfanyi kuonekana mnyonge bali kujiongezea kukubalika na ushawishi kwa wale utakao waongoza.

JIFUNZE KUWASILIANA VYEMA

Uhusiano wowote ule unaimarika kupitia mawasiliano thabiti na ya uhakika. Vivyo hivyo katika uongozi, mawasiliano ni moja ya vitu muhimu sana na watu wanaofanikiwa katika kuwasiliana huwa na moja ya sifa muhimu ya kiongozi bora.

Jifunze kutafuta na kutoa taarifa sahihi na kwa wakati  kwa wengine.

KUWA MTENDAJI NA SI MTOA MAELEKEZO

Watu wengi hufikiri kuwa, kiongozi unachotakiwa kufanya ni kutoa amri na maelekezo juu ya nini kinatakiwa kifanywe lakini ukweli ni kwamba kiongozi mzuri ni yule aliyepo katika mchakato wa kufanya.

Usiseme “fanyeni hivi” bali “tufanye hivi”. Viongozi wenye kutoa maelekezo pekee katika taasisi hukumbana na upinzani mkubwa ambao si mzuri katika kufanikisha malengo ya kiuongozi na ya kitaasisi.

ZINGATIA UTU

Kufanya kazi na watu hasa watu wazima kunahitaji hekima sana. Kuna uwezekano ukapewa dhamana ya kuwaongoza watu waliokuzidi vitu vingi ikiwamo elimu, uzoefu na hata umri.

Jifunze kuchunga kauli zako unazozitoa juu yao iwe hadharani na hata kwa faragha. Kuwa mfariji na mtu wa kutia moyo unayejali fikra za watu na unapoonya, onya kwa hekima.

KUWA MTATUA MATATIZO NA MTU WA MATOKEO

Kiongozi anaaminika kuwa ni mtu mwenye uwezo wa juu zaidi ya wengine na ndiyo maana si wote wanaopewa uongozi bali ni wateule wachache tu. Sasa nini kitakufanya uwe wa tofauti?

Jifunze kuwa na mbinu za kukabiliana na matatizo na changamoto zinazoikabili timu yako na kushirikiana nao katika kuzikabili. Kuwa tayari kutoa mawazo na kukubali maoni ya wengine juu mawazo yako.

JIAMINI

Watu wengi hujikuta katika mazingira ambayo wanatilia shaka uwezo wao. Jifunze kujiamini na hili lionekane unapoongea na kwa yale unayoyafanya. Hakuna atakayekubali kuongozwa na mtu asiyeamini uwezo wake mwenyewe.

Kelvin Mwita ni Mhadhiri Msaidizi Chuo Kikuu Mzumbe, anapatikana kwa 0659 08 18 38, [email protected], www.kelvinmwita.com

 

Habari Kubwa