Silaha iliyoibwa mkesha wa Krismasi yakamatwa

08Jan 2017
Robert Temaliwa
BAGAMOYO
Nipashe Jumapili
Silaha iliyoibwa mkesha wa Krismasi yakamatwa

JESHI la Polisi limekamata silaha aina ya SMG na risasi 30 iliyokuwa imeibwa siku ya mkesha wa Krismasi katika lango la Gama kwenye Hifadhi ya Taifa ya Saadani, Makurunge Wilayani Bagamoyo.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Bonaventura Mushongi.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Bonaventura Mushongi, alisema jana kuwa silaha hiyo pamoja na risasi 30, iliibwa kutoka kwa askari Jackson Shirima (23), mkazi wa Hifadhi ya Taifa ya Saadani, akiwa kazini.

Mushongi alisema silaha hiyo na risasi vimekamatwa kutokana na ushirikiano wa Jeshi la Polisi, Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (Tanapa) na hifadhi ya Saadani.

Alisema silaha hiyo imepatikana baada ya mtuhumiwa mmoja, Swalehe Mangupili (39), mkazi wa Tegeta Kibaoni, Dar es Salaam kwenda kuonyesha alikokuwa ameificha katika kichaka eneo la Mto Kitame, Kijiji cha Gama wilayani Bagamoyo.


Aidha alisema operesheni ya kusaka wahalifu iliyofanyika juzi kwa nyakati tofauti huko Ruvu Darajani, imefanikisha kuwakamata watuhumiwa wanne wakiwa na bangi viroba 17 na kete 590.

Mushongi pia alisema katika operesheni hiyo, walimkamata mtuhumiwa mmoja akiwa na pombe haramu ya gongo lita tano.

Ili kufanikisha mapambano dhidi ya uhalifu wa aina mbalimbali, Kamanda Mushongi 
aliwataka wananchi mkoani hapa kutoa ushirikiano kwa jeshi hilo kwa kutoa taarifa za wahalifu katika maeneo wanayoishi ili hatua za haraka zichukuliwe dhidi yao.

Habari Kubwa