Silaha yatelekezwa ofisi ya serikali ya mtaa

01Aug 2020
Nebart Msokwa
Mbeya
Nipashe
Silaha yatelekezwa ofisi ya serikali ya mtaa

KATIKA hali isiyokuwa ya kawaida, silaha aina ya bastola imeokotwa ikiwa imetelekezwa na watu wasiojulikana nje ya Ofisi za Serikali ya Mtaa wa Maendeleo katika Kata ya Iyela, jijini Mbeya.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mbeya, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi, Ulrich Matei, picha mtandao

Jeshi la Polisi pia linamshikilia mzee mmoja Amani Mpendule (68), mkazi wa Kata ya Lualaje, wilayani Chunya kwa tuhuma za kukutwa na bunduki aina ya gobore iliyotengenezwa kienyeji bila kuwa na kibali.

Akizungumza na waandishi wa habari ofsini kwake jana, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mbeya, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi, Ulrich Matei, alisema katika tukio la kwanza maofisa wa jeshi hilo waliiokota bastola hiyo aina ya Taurus ambayo imetengenezwa nchini Brazil.

Alisema bastola hiyo ina namba za usajili TGT.10582/PT 809 ambayo mmliliki wake hajafahamika na kwamba jeshi hilo linaendelea kufanya uchunguzi ili kubaini mmiliki wa silaha hiyo.

“Bastola hii iliokotwa Julai 25, mwaka huu, sasa unapokuta silaha kama hii katika mji huu ujuwe hata wahalifu wapo, hivyo tunaomba mtu yeyote ambaye anamfahamu mmiliki wa silaha hii atoe taarifa ili tuwakomeshe wahalifu hawa,” alisema Kamanda Matei.

Katika tukio la pili, Kamanda Matei alisema Mpendule alikamatwa na gobore hilo ambalo analimiliki bila kuwa na kibali akiwa anaendelea kulitumia kwenye uwindaji haramu katika Hifadhi ya Taifa ya Ruaha.

Alisema mzee huyo alikamatwa wakati wa msako wa pamoja kati ya maofisa wa Jeshi la Polisi na maofisa wa Mamlaka ya Hifadhi za Taifa (TANAPA) kwenye maeneo mbalimbali ya Wilaya ya Chunya.

Alisema mbali na mtuhumiwa huyo kukamatwa na bunduki hiyo pia alikutwa akiwa na vipande vya nondo na baruti ambavyo alikuwa anavitumia kuua wanyama kwenye hifadhi hiyo.

“Tunaendelea kumhoji mtuhumiwa na ushahidi utakapokamilika tutamfikisha mahakamani kwa ajili ya hatua zaidi za kisheria, hivyo natoa tahadhari kwa watu wote wanaomiliki silaha bila kuwa na vibali kuzisalimisha haraka katika Jeshi la Polisi,” alisema Kamanda Matei.

Alisisitiza kuwa jeshi hilo litafanya msako wa nyumba kwa nyumba ili kuhakikisha watu wote wanaomiliki silaha bila kuwa na vibali wanakamatwa na kushughulikiwa kwa mujibu wa sheria.

Habari Kubwa