Alisema hayo jana baada ya kutembelea miradi ya ujenzi wa mabweni katika Halmashauri za Bariadi na Itilima mkoani Simiyu.
Silinde alisema kutokana na ushauri mbaya unaotolewa na wahandisi hao, miradi mingi haikamiliki kutokana na kutozingatia bajeti inayopangwa na serikali kuu.
Katika miradi ya ujenzi wa mabweni inayojengwa katika halmashauri hizo, Silinde alikuta haijakamilika huku wahandisi wakilalamikiwa kwa kutoa makisio ya bei za juu ya ujenzi kuliko hali halisi ya ujenzi.
"Nimepita katika halmashauri zingine gharama ile tuliyotoa ya Sh. milioni 80 imemaliza ujenzi kwa kuwa baadhi ya wakuu wa shule walibana matumizi na kusimamia vizuri fedha walizopewa," alisema.
Silinde alisema kuwa katika maeneo mengine, wengi walioshindwa kumaliza, walifuata ushauri wa wahandisi wasio wazalendo kwa serikali yao, ambao walipotosha na kuweka gharama kubwa zaidi na kufanya walimu kuingia matatizoni kwa matumizi mabaya ya fedha.
Mkuu wa Wilaya ya Bariadi, Festo Kiswaga, amemwahidi Silinde kuwa mpaka ifikapo Mei, mwaka huu, majengo yote ya mabweni yatakuwa yamekamilika kwa fedha za ndani baada ya fedha walizoletewa na serikali katika shule mbili wilayani kwake kwa ajili ya ujenzi wa mabweni Sh. milioni 160 kushindwa kumaliza mradi huo.
Katika hatua nyingine, Silinde aliwaagiza wakuu wa shule za sekondari za Itilima, Bariadi na Nyasosi na maofisa elimu sekondari wilaya za Bariadi na Itilima kuandika barua kujieleza kwanini wasichukuliwe hatua kwa kuchelewa kumaliza ujenzi wa mabweni katika shule hizo.
Silinde alisema endapo watashindwa kukamilisha majengo hayo kwa muda walioomba kuongezewa, basi atawavua nyadhifa zao.