Silinde atimkia CCM

06Jul 2020
Elizaberth Zaya
Dar es Salaam
Nipashe
Silinde atimkia CCM

ALIYEKUWA Mbunge wa Momba mkoani Songwe, David Silinde, jana alikabidhiwa rasmi kadi ya uanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Silinde alikabidhiwa kadi hiyo pamoja na wanachama wengine waliohama kutoka Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) na kujiunga CCM.

Tukio hilo lilifanyika Tunduma mjini mkoani Songwe, katika hafla maalum ya kumkabidhi Silinde na wenzake kadi hizo zilizokabidhiwa na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Huphrey Polepole.

Silinde ni miongoni mwa wabunge ambao walifukuzwa uanachama wa CHADEMA baada ya kugoma kutii agizo la chama lililotolewa na chama hicho la kujitenga kwa siku 14 bila kuingia bungeni kwa ajili ya kuchukua tahadhari ya ugonjwa wa corona.

Mbali na Silinde, wengine waliofukuzwa uanachama ni aliyekuwa Mbunge wa Moshi Vijijini, Antony Komu, Joseph Selasini (Rombo) na Wilfred Lwakatare(Bukoba Mjini), ambao wote walikihama chama hicho baada ya bunge kuvunjwa.

Katibu Mkuu wa CHADEMA, John Mnyika, akitangaza kuwafukuza uanachama wabunge hao, alisema uamuzi huo ulitokana na kikao cha Kamati Kuu kilichokaa kuwajadili na kubaini kwamba walipoteza sifa ya uanachama baada ya kukaidi agizo la chama na kujitangazia mbele ya vyombo vya habari kwamba hawakukubaliana na itikadi za CHADEMA.

CHADEMA pia kilidai kwamba mbali na kujitangaza, lakini walikuwa wakitumia maneno ya kejeli na kashfa kwa viongozi wa chama hicho.

Habari Kubwa