Simanzi kuagwa miili wanahabari Azam Media

10Jul 2019
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Simanzi kuagwa miili wanahabari Azam Media

HALI ya huzuni, vilio na simazi ilitawala katika viwanja vya ofisi Kampuni ya Azam Media jijini Dar es Salaam jana, wakati wa ibada ya kuanga miili ya wafanyakazi watano wa kampuni hiyo waliokufa kwa ajali juzi mkoani Singida.

Magari matano yaliyobeba miili yanayowasili katika viwanja hivyo vilivyo Tabata TIOT barabara ya Mandela. Wakati majeneza yanashushwa kwa mpangilio wa aina yake, ndugu jamaa na marafiki kadhaa waliokuwapo waliangua vilio kwa uchungu.

Wafanyakazi waliokufa katika ajali iliyohusisha gari aina ya Toyota Coaster waliyokuwa wamepanda wakisafiri kikazi kuelekea Chato, mkoani Geita iliyogongana ana na lori. Waliokufa ni Salim Mhando, Charles Wandwi Florence Ndibalema, Sylvanus Kasongo na Said Haji.

Wafanyakazi hao watano ni miongoni mwa watu saba waliofariki katika ajali hiyo. Vifo hivyo vimetajwa kutonesha mioyo ya wanatasnia ya habari, wengi walia kuwa umekuwa ni mwaka mgumu kutokana na vifo kadhaa vya wanatasnia wakiwamo nguli vilivyotokea tangu mwaka huu uanze.

Baadhi ya wanatasnia waliofariki dunia mwaka huu ni pamoja na Mwenyekiti Mtendaji wa IPP, Dk. Regnald Mengi, Mkurugenzi wa vipindi wa Clouds Media Group, Ruge Mutahaba, Mwandishi wa Radio One na ITV ambaye pia alikuwa Makamu Mwenyekiti wa Arusha Press Club, Charles Ngereza Mwandishi wa Mwananchi Shaaban Ndyamkama.

JOYCE MHAVILE

Akizungumza kwa niaba ya vyombo binafsi vya habari nchini, Joyce Mhavile, Mkurugenzi Mtendaji wa ITV na Redio One, alisema vifo hivyo vimeufanya mwaka huu uendelee kuwa mgumu kwa waandishi wa habari.

“Msiba huu umetupiga kwenye tasnia ya habari mwaka huu umekuwa mgumu sana, lakini nawasihi ninyi ambao mmebaki wafanyakazi wa Azam mhakikishe mnafanya kwa bidii kuziba pengo,” alisema Muhavile.

HUMPHREY POLEPOLE

Katibu wa Itikadi na Uenezi CCM, Humphrey Polepole, alisema tasnia ya habari huu ni msiba mwingine mkubwa kwa mwaka huu.

Alisema kuwa ni jambo linaloumiza kuwa vijana walikuwa wadogo, wamesoma wameelimika walianza kulitumikia taifa wamepata msiba wakiwa kazini.

Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe, alisema anakubaliana na wengine kwamba mwaka huu tasnia ya habari imepata mishtuko mikubwa mingi mizito.

“Ni ushuhuda ulio wazi kuwa tasnia ya habari inapoguswa nchi nzima inatikisika ni ushuhuda tu wa umuhimu wa vyombo vya habari katika nchi yetu, ni ushuhuda jinsi ambavyo vyombo vya habari vinapewa uzito katika taifa namna ambavyo vyombo vya habari vinawajibu wa kipekee katika kulijenga ama kulibomoa taifa,” alisema Mbowe.

Mbowe ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chadema alibainisha kuwa: “Taifa letu tunaopenda tunastahili kupendana zaidi, vyombo vya habari ni kiunganishi kizuri sana katika kujenga umoja na mshikamano na upendo katika taifa letu,lakini tukiruhusu vyombo vya habari vitumike kutugawa tutagombana,tutalaumiana tutauma mapendo na mshikamano wetu.” alisema.

Aliwasihi viongozi wote wenye mamlaka ya kusimamia vyombo vya habari kuhakikisha wanasimamia vifanye kazi kwa weledi visitumike vibaya, hatua ambayo itasaidia katika kujenga taifa bora.

DK. MWAKYEMBE

Serikali imetumia nafasi hiyo kutoa onyo la mwisho kwa wamiliki wa simu za mkononi za kisasa(smart phone) wenye tabia ya kupiga picha za maiti katika matukio ya ajali.

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk. Harrison Mwakyembe, alitoa onyo hilo wakati akizungumza kwa niaba ya serikali katika ibada hiyo.

Alisema kuna watu wamepoteza utu inapotokea ajali wanakimbilia kupiga picha za miili ya wahusika na kuzisambaza kwenye mitandao ya jamii.

MASAUNI

Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Masauni, alibainisha kuwa tayari dereva wa lori ambaye alikimbia baada ya ajali hiyo amekamatwa na polisi.

Mkuu wa kikosi cha usalama barabarani nchini, Fortunatus Muslim alisema amesikitishwa na ajali hiyo kwa kuwa vijana hao wamekuwa wakishirikiana na kikosi hicho katika kuelimisha jamii masuala ya usalama wa barabarani.

“Tumepoteza wataalam ambao walikuwa na nguvu za kufanya kazi, tulikuwa tunafanya nao kazi za usalama barabarani.

BOSI TRAFIKI

Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani, Fortunatus Muslim, alisema ajali imewakuta wakiwahi kwenye matukio kule Chato walikuwa ni wachapakazi wanaopenda taaluma yao baadaye wangekuwa ni nguli kwenye masuala ya tasnia.

Aliwataka madereva waone kuwa wana dhamana kubwa wamebeba roho na maisha ya watu, wataendelea kuwadhibiti madereva ambao hawafuati sheria za usalama barabarani.

Watu mbalimbali wakiwamo viongozi kutoka Serikali walihudhuria msiba huo,miongoni mwao ni Waziri wa Muungano na Mazingira January Makamba, viongozi wa taasisi za habari ikiwamo Baraza la Habari Tanzania(MCT).

Wengine ni kutoka Jukwaa la Wahariri (TEF) na Chama cha Waandishi wa habari Wanawake (TAMWA) na Chama cha wamiliki wa vyombo vya habari nchini MOAT na waandishi wa habari kutoka katika vyombo mbalimbali vya habari nchini.

Mmiliki na Mwenyekiti wa makampuni ya Bakhresa, Said Salim Bakhresa, Mwenyekiti wa CUF, Prof. Ibrahimu Lipumba, Kiongozi Mkuu wa ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe, Naibu katibu Mkuu wa chama hicho, Magdalena Sakaya ambaye pia ni Mbunge wa Kaliua.

MAJERUHI

Mkuu wa Idara ya magonjwa ya dharura wa Hospitali ya Arusha Lutheran Medical Centre (ALMC), Dk. Richard Mabula, amesema hospitali hiyo imepokea majeruhi wawili juzi kati ya watatu ambao ni wafanyakazi wa Azam Media Limited.

Alisema juzi, walipigiwa simu na kampuni ya ndege ya Arusha Medivac Ltd, kwa lengo la kwenda mkoani Singida, Hospitali ya Wilaya ili kusaidia uokoaji wa majeruhi hao watatu.

Alisema walipofika majira ya mchana Singida waliambiwa majeruhi hao wamehamishiwa hospitali ya Nkinga na baada ya kufika, waliwachukua majeruhi wawili ambao hali zao zilikuwa mbaya huku mmoja akiendelea kutibiwa hospitali hapo.

Alisema baada ya kuwachukua majeruhi hao ambao ni Wahandisi Datus Masawe na Mohamed Mahige, walishauriana kuwapeleka Hospitali ya Bugando Mwanza, Dar es Salaam au Arusha.

Vile vile, alisema rubani wa ndege hiyo (hakumtaja jina) aliona wakienda jijini Dar es Salaam watachukua saa tatu angani lakini wakienda Arusha watachukua saa moja angani.

"Hivyo tulikubaliana kuwaletea Arusha ili tusitumie muda mrefu angani katika kuokoa maisha yao," alisema.

Mkurugenzi wa Huduma na Tiba wa hospitali hiyo, Gofrey Kibira, alisema wagonjwa hao wawili wanaendelea na matibabu na wameumia maeneo mbalimbali ya miili yao, haswa maeneo ya mifupa shingoni, usoni, miguu na mikono.

Alisema mpaka jana hali zao zinaendelea vizuri na jana mchana waliwapeleka chumba cha upasuaji ingawa mgonjwa mmoja kati ya wawili hao anaongea vitu visivyotambulika.

 Imeandikwa na Beatrice Moses, Dar Salome Kitomari na Cynthia Mwilolezi, Arusha

Habari Kubwa