Simba ilivyoiteka Afrika kipigo AS Vita U/Taifa

18Mar 2019
Adam Fungamwango
DAR ES SALAAM
Nipashe
Simba ilivyoiteka Afrika kipigo AS Vita U/Taifa

HISTORIA imeandikwa baada ya Klabu ya Simba ya Tanzania kutinga hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa kuibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya timu ngumu ya AS Vita.

Kiungo wa Simba, Claotus Chama (kushoto), akishangilia sambamba na John Bocco, baada ya kuifungia timu yake bao la pili dhidi ya AS Vita kwenye Uwanja wa Taifa juzi.

Mechi hiyo kali iliyochezwa Jumamosi kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, ilikuwa ya mwisho kwenye Kundi D, Simba ikikamata nafasi ya pili ikiwa na pointi tisa, nyuma ya Al Ahly ya Misri iliyomaliza nafasi ya kwanza kwa kukusanya pointi 10.

Timu za JS Saoura ya Algeria na AS Vita zimetupwa nje ya michuano hiyo.

Hii ni mara ya kwanza kwa Simba kuifunga AS Vita baada ya kucheza nao mara tano.

Mara ya kwanza ilikuwa ni 1978 kwenye mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika, Simba ikachapwa bao 1-0 jijini Dar es Salaam na kufungwa tena bao 1-0 kwenye mechi ya marudiano nchini DR Congo, zamani ikiitwa Zaire.

Mara ya tatu timu hizo zilikutana kwenye michuano ya Kombe la Kagame mwaka 2012 iliyofanyika nchini na zikatoka sare ya bao 1-1, mara ya nne ilikuwa kwenye mechi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa zilipokutana DR Congo na Simba kuchapwa mabao 5-0.

Hata hivyo, Simba bado haijaifikia rekodi yake iliyoweka mwaka 1974 ilipofanikiwa kutinga hatua ya nusu fainali na kutolewa na Mehalla El Kubra ya Misri kwa mikwaju ya penalti baada ya kila moja kushinda kwake bao 1-0.

Yafuatayo ni mambo yaliyojitokeza kwenye mechi hiyo ambayo imeiingiza timu hiyo kwenye vitabu vya kumbukumbu...

 

1. AS Vita iliingia kwa nguvu moja

Mechi ilipoanza tu, AS Vita ilianza kwa kasi na lengo lilikuwa ni  kupata bao la mapema ambalo lingeichanganya Simba na  haikushangaza walipopata bao la mapema, dakika ya 13 tu kupitia kwa Kazadi Kazengu.

 

2. Simba walifungwa bao kama la Lipuli

Kama ulitazama mechi kati ya Simba dhidi ya Lipuli iliyochezwa kwenye Uwanja wa Samora mjini Iringa, halikutofautiana sana na lile la juzi dhidi ya AS Vita.

Mabeki wa Simba wanatatizo la kucheza na refa kwa kunyoosha mikono, huku wakiomba huruma, wakiuacha mpira na wenzao wanawaadhibu kwa njia hiyo.

Kwenye mechi ya Lipuli, mchezaji mmoja alianguka wakanyoosha mikono huku wamesimama, lakini yule yule aliyeanguka alimpasia  mfungaji na kuuweka wavuni, ingawa Simba ilishinda mabao 3-1.

Mechi dhidi ya AS Vita, Erasto Nyoni alionekana kuangushwa na straika wa wapinzani wao, mabeki wa Simba badala ya kuuondoa kwanza, wakainua mikono juu, wakiomba huruma ya refa, wakaadhibiwa.

 

3. Mabao kufungwa na wasiotarajiwa

Kwenye mechi hiyo ya kihistoria, mabao ya Simba yalifungwa na wachezaji ambao hawakutarajiwa kabisa na mashabiki.

Mohamed Hussein 'Tshabalala' alifunga bao la kwanza, mchezaji ambaye ni aghalabu sana kufunga bao hata kwenye mechi za Ligi Kuu Tanzania au michuano mingine yoyote ile.

Pamoja na Clatous Chama kuwa mchezaji bora na aliyeiingiza Simba kwenye hatua ya makundi kwa bao lake dhidi ya Nkana FC, lakini hakuna aliyetarajia kuwa angeweza kuwa mkombozi kwa mara nyingine tena.

Ni kwa sababu kwa siku za karibuni Chama ameonekana hayupo kwenye kiwango chake kilichozoeleka, lakini ni yeye ambaye bao lake la dakika za mwishoni lililoipeleka Simba robo fainali kama alivyoiingiza kwenye hatua ya makundi.

 

4. Niyonzima aliwavuruga Wakongomani

Moja kati ya mabadiliko aliyoyafanya kocha wa Simba ni kumtoa Emmanuel Okwi ambaye hakuwa kwenye kiwango chake cha kawaida na kumuingia Haruna Niyonzima.

Mabadiliko hayo kwa kiasi kikubwa ndiyo yaliwavuruga na kuwaumiza kabisa Wakongomani hao.

Simba ilikuwa inacheza na viungo watatu, huku AS Vita ikiwa na viungo wanne, hivyo wageni hao walitawala kati.

Lakini baada ya kuingia Niyonzima, akabadilisha kabisa mwenendo wa mchezo na kuifanya timu yake itawale kati kwa kiasi kikubwa.

Uwezo wa kuuchezea mpira atakavyo, pasi za haraka  zisizotabirika kuwa zitakwenda kwa nani, unyumbulifu wa hali ya juu na ubunifu, uliwafanya viungo wa AS Vita kupoteana kabisa na kuwapa nafasi viungo wa Simba kutamba na kufanikiwa kupata bao la pili dakika ya 90.

 

5. Erasto aliituliza beki Simba

Beki ya Simba ilikuwa kwenye wakati mgumu alipokuwa ameumia Erasto Nyoni na inawezekana kabisa ndiyo ilisababisha Simba kufungwa  mabao 5-0 dhidi ya AS Vita na Al Ahly ugenini, lakini kwenye mechi ya Jumamosi alikuwa ndani ya dimba na umuhimu wake ulionekana licha ya kuwa huo ulikuwa mchezo wa kwanza kwake kucheza tangu atoke kwenye chumba cha majeruhi.

Nyoni aliituliza kabisa safu ya ulinzi ya Simba ambayo mara nyingi hukatika na hasa inapokutana na timu zenye mastraika wanyumbulifu na wenye kasi, lakini kwenye mechi hiyo ilitulia, huku akifuta makosa ya wenzake, akicheza kwa ufundi na utulivu wa hali ya juu.

Habari Kubwa