Simbachawene aagiza tathmini mpya madawati

27Jun 2017
Augusta Njoji
MPWAPWA
Nipashe
Simbachawene aagiza tathmini mpya madawati

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), George Simbachawene, ameziagiza Halmashauri zote nchini kufanya upya tathmini ya madawati katika Shule za Msingi ili kujua mahitaji halisi kwa sasa.

George Simbachawene.

Simbachawene alitoa kauli hiyo alipofanya ziara ya kukagua miradi ya maendeleo katika Wilaya ya Mpwapwa.

Alisema kwa mujibu wa taarifa alizopelekea, madawati yanatosheleza, lakini tathmini aliyoifanya wilayani humo inaonekana kuna upungufu.

“Katika taarifa nilizoletewa mimi madawati yametosheleza na yamepitiliza, lakini nilichokuja kukiona baada ya kufanya tathmini kwa Wilaya ya Mpwapwa bado tunaupungufu wa madawati katika shule za msingi nyingi,” alisema.

Alitaka tathmini iendelee kufanyika kwa kufika kwenye madarasa na kuangalia kama watoto wanakaa kwenye madawati.

“Kwa sababu inawezekana taarifa mlizotuletea ni za uongo kwa sababu kwa Mpwapwa mlisema yamekamilika, lakini Mkuu wa wilaya upungufu huu ni mkubwa, nimeleta madawati 120 mbona yanagombaniwa maana yake ni upungufu mkubwa,” alisema Simbachawene.

Hivi karibuni, Simbachawene akisoma hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara yake Bungeni kwa mwaka 2017/18, alisema hadi  kufikia Desemba, 2016 baada ya utekelezaji wa agizo la Rais John Magufuli la kuhakikisha kila mwanafunzi anakaa kwenye dawati, mikoa yote ilijitosheleza kwa madawati na kuwa na ziada.

Aidha, alisema kutokana na uandikishaji na usajili wa wanafunzi wa darasa la awali, darasa la kwanza na kidato cha kwanza mwaka 2017, hadi Machi kumekuwapo na upungufu wa madawati 302,787 kwa shule za msingi na madawati 204,526 kwa shule za sekondari nchini.

Katika ripoti yake ya 2015/16 aliyoikabidhi kwa Rais John Magufuli Machi 27, mwaka huu, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), anabainisha uhaba mkubwa wa samani na miundombinu katika shule za msingi nchini, hali inayosababisha wanafunzi kufanya vibaya kwenye masomo yao.

Ripoti hiyo iliyowasilishwa bungeni Aprili 13, mwaka huu, inaeleza licha ya serikali kufanya kampeni kubwa ya utengezaji madawati, ukaguzi wake umebaini wanafunzi milioni 1.1 hawana madawati, sawa na asilimia 13 ya mahitaji.

Inaongeza kuwa kutokana na kampeni hiyo, upatikaji wa madawati umeimarika kutoka upungufu wa asilimia 24 mwaka 2015 hadi asilimia 13 mwaka jana.

Habari Kubwa