Simbachawene atoa siku 90 TSC kuwaondoa wala rushwa

20Dec 2016
Paul Mabeja
Dodoma
Nipashe
Simbachawene atoa siku 90 TSC kuwaondoa wala rushwa

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), George Simbachawene, ametoa miezi mitatu kwa Mwenyekiti wa Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC), Oliver Mhaiki, kuwaondoa watumishi wanaotuhumiwa kula rushwa ili chombo hicho kiwe na tija kwa walimu.

Akizungumza wakati wa uzinduzi na kuwaapisha wajumbe wa tume hiyo mjini hapa jana, Simbachawene alisema watumishi hao wanaopaswa kuondolewa ni wale waliowarithi kutoka Idara ya Huduma ya Walimu (TSD) ambao wamelalamikiwa kuwaomba rushwa walimu.

“Hatuwezi kuendelea na watu wale wale ambao walikuwa wanafanya kazi katika chombo hicho, hivyo basi nikuagize Mwenyekiti ndani ya miezi mitatu uwe tayari umeshapitia watumishi wote walio katika Tume hii kuwabaini wapenda rushwa na wabadhirifu ili chombo hiki kiwe chenye tija,” alisema Simbachawene.

Alifafanua kuwa kumekuwapo na malalamiko ya watu kuomba rushwa ili majalada yao ya kesi yasikilizwe, hali ambayo inasababisha wengine kukosa haki zao.

“Unakuta mtu anaambiwa atoe pesa kwanza ndipo jalada lake lisikilizwe, sasa hapo kweli unatarajia katika kesi hiyo nani atashinda kama siyo yule mwenye fedha?,” Alisema na kuhoji Waziri Simbachawene.

Alisema kuwa chombo hicho ni muhimu katika kutetea maslahi ya walimu pamoja na kuhakikisha kuwa elimu inayotolewa nchini inakuwa bora.

Aliwataka wajumbe hao walioteuliwa kuhakikisha wanafanya kazi zao kwa mujibu wa kanuni na sheria zilizowekwa na mamlaka husika.

“Hatuwezi kuvumilia kuona kuwa ofisi ya serikali kama hii inakuwa kama kijiwe cha majambazi, watu wanaomba rushwa, vurugu tupu kama mapaka fulani hivi,” alisema Simbachawene.

Alisema kuwa watumishi katika chombo hicho watakaobainika kuwa si waadilifu, wasipatiwe nafasi, bali watafutwe watu ambao ni waadilifu na watakaofanya kazi kwa ufanisi.

Kwa upande wake, Katibu wa tume hiyo, Winfrida Rutaindurwa, alisema tume hiyo inakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwamo upungufu wa watumishi.

“Upungufu wa watumishi katika wilaya zote na mikoa nchini, ni 776, lakini waliopo ni 463, pia hatuna gari hata moja katika ofisi za wilaya hali ambayo ni changamoto kubwa katika utendaji wetu wa kila siku,” alisema Rutaindurwa.

Habari Kubwa