Simiyu yapiga hatua vita dhidi ya malaria

28Feb 2019
Happy Severine
Simiyu
Nipashe
Simiyu yapiga hatua vita dhidi ya malaria

KAIMU Mganga Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Dk. Mguna Maeka, amesema ingawa hali ya maambukizi ya ugonjwa wa malaria bado si nzuri, mkoa huo  umepunguza kiwango cha maambukizi hayo hadi kufikia asilimia  6  kwa mwaka 2017 kulinganisha na asilimia 13.4 ya mwaka  2015/16.

kaimu mganga mkuu wa Mkoa wa Simiyu Mguna Maeka katikati ,(aliyesimama) akitoa taarifa fupi ya hali halisi ya ugonjwa wa malaria Simiyu,kushoto ni Linda Nakara kutoka mpango wa Taifa wa kudhibiti malaria ,kushoto ni Hamid All Away kutoka katika shirika la T MARC

Dk. Maeka alisema hayo jana wakati wa kikao cha utambulisho wa mradi wa ‘badili tabia, tokomeza malaria’ mkoani Simiyu, uliofanyika katika ukumbi wa Sweet Dream mjini hapa.

Alisema pamoja na  ugonjwa huo kusumbua jamii na nchi kwa ujumla, kumekuwapo na mafanikio makubwa katika utekelezaji wa mikakati ya kupambana nao.

Mganga mkuu aliongeza kuwa mafanikio hayo yametokana na juhudi za serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali katika kuhakikisha mikakati hiyo ya udhibiti inatekelezwa kwa ufanisi.

Naye Mwakilishi wa Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhandisi Hatari Kapufi, alisema mbali na kupungua kwa maambukizi ya malaria, bado juhudi kubwa zinatakiwa kufanyika ili kupunguza kiwango cha sasa na kufikia asilimia moja na hatimaye kutokomeza kabisa ugonjwa huo ifikapo mwaka 2030.

Kwa upande wake Ofisa Ufuatiliaji na Tathmini wa shirika la T- MARC, Levina Thobias, alisema mradi wa Badili Tabia, Tokomeza Malaria, unatarajia kuanza Machi, mwaka huu na kufikiwa jumla ya walengwa 2,000.

Thobias alisema mradi huo unawalenga hasa wajawazito, wanyonyeshao na watoto chini ya umri wa miaka mitano ambao ndio mara nyingi waathirika wa malaria.

Aliongeza kuwa mradi huo unaotekelezwa na shirika lake chini ya ufadhili wa GSK (Comic Relief Malaria Initiative with Gloxosmithkine) utatekelezwa mkoani Simiyu kwa kipindi cha miaka miwili na matarajio yao ni kupunguza kabisa na kutokomeza malaria.

Habari Kubwa