Simiyu yapokea kitabu cha mwongozo wa kilimo cha mkonge

13Sep 2020
Happy Severine
Simiyu
Nipashe
Simiyu yapokea kitabu cha mwongozo wa kilimo cha mkonge

​​​​​​​BODI ya Mkonge nchini imekabidhi kitabu cha muongozo wa kilimo cha mkonge kwa wadau wa kilimo hicho mkoani Simiyu ili kuhakikisha kila mkulima anazalisha mkonge ulio na ubora na kuuza kwa thamani zaidi sokoni.

Mratibu Mkuu wa Utafiti na Masoko wa zao la mkonge, Hassan Kibarua(wa pili kutoka kulia) akimkabidhi Katibu Tawala wa Mkoa wa Simiyu Mariam Mmbaga(wa pili kushoto) kitabu cha mwongozo wa kilimo cha mkonge.

Akikabidhi muongozo huo leo kwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Simiyu, Mariam Mmbaga, Mratibu Mkuu wa Utafiti na Masoko, Hassan Kibarua, amesema kuwa mkonge unaozalishwa kanda ya ziwa ni mrefu zaidi hivyo inatakiwa wakulima waelimishwe namna ya kuuchakata kwa utaalam ili usipunguze thamani.

Kibarua amesema mkonge unatakiwa kuchakatwa si zaidi ya masaa 48 tangu umekatwa lakini wakulima wengi wanachakata mkonge huo  uliokatwa zaidi ya siku tano hali inayosababisha mkonge huo kupungua  ubora wake unapofika sokoni .

Ameongeza kuwa wakulima wanatakiwa kuelezwa namna ya kuchakata na kusafisha mkonge ili wasiupeleke sokoni ukiwa mchafu (maganda) kwani makosa ukiwa na dosari kidogo unashuka thamani yake halisi.

Awali akieleza umuhimu wa kupima afya ya udongo ili kuongeza uzalishaji wa mkonge, Mratibu wa Utafiti wa UdongoTanzania kutoka TARI- Mlingano Dr Sibaway Mwango, asema kuwa maafisa ugani wawe ni daraja la kuwaunganisha watafiti na wakulima.

Nao baadhi ya wakulima wa Mkonge Mkoani Simiyu wameeleza namna ambavyo wanaendesha kilimo hicho na kuwa hapo awali hawakujua kuwa mkonge ni mali hadi walipo pata elimu ya kilimo hicho na kuifanyia kazi ambapo kwa  sasa wameanza kunufaika.

Katika Mkoa wa Simiyu zao la mkonge tayari limeanza kulimwa na wakulima katika baadhi ya maeneo hasa katika Wilaya ya Meatu na Maswa ambao hupeleka mkonge huo katika shirikisho la wakulima wa mkonge Kishapu (SHIWAMKI) mkoani Shinyanga.

Habari Kubwa