Simu ya mpenzi ilivyomponza mwanafunzi UDSM aliyepotea

14Mar 2018
Romana Mallya
DAR ES SALAAM
Nipashe
Simu ya mpenzi ilivyomponza mwanafunzi UDSM aliyepotea

JESHI la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, limesema mwanafunzi wa mwaka wa tatu Kitivo cha Sayansi ya Siasa na Utawala (UDSM), Abdul Nondo, aliyeripotiwa kutekwa na kusababisha taharuki, uchunguzi umebaini hakutekwa bali alikwenda kwa mpenzi wake Iringa.

Nondo ambaye pia ni Mwenyekiti wa Mtandao wa Wanafunzi Tanzania (TSNP), mwanzoni mwa wiki iliyopita aliripotiwa kutoweka katika mazingira ya kutatanisha baada ya kuwaaga wanafunzi wenzake kuwa anaelekea nyumbani kwao, Madale na baadaye kutuma ujumbe kuwa, yupo hatarini.

Kamanda wa Kanda hiyo, Lazaro Mambosasa aliwaambia waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam kuwa, uchunguzi uliohusisha polisi Dar es Salaam na Iringa, umebaini mwanafunzi huyo hakutekwa bali alijiteka.

Alisema muda ambao mwanafunzi huyo aliotuma ujumbe mfupi kuwa yupo hatarini simu yake ilionyesha alikuwa akiwasiliana na mpenzi wake aliyeko Iringa.

Kamanda Mambosasa alisema uchunguzi uliofanyika umeonyesha mwanafunzi huyo hakutekwa bali alijiteka mwenyewe na kuamua kutoa taarifa zikiwa na maslahi binafsi.

Akisimulia kuhusu tukio hilo, Kamanda alisema baada ya kusambaa kwenye mitandao ya kijamii, jeshi hilo lilianza ufuatiliaji.

"Katika ufuatiliaji huo tulilenga kubaini ukweli juu ya tukio hili ambalo tayari lilishatolewa taarifa na mitandao hiyo ya kijamii, tulifungua jalada namba DSM/KINO/CAD/PE/51/2018," alisema.

Kamanda Mambosasa alisema Machi 7 walipata taarifa kutoka Iringa kwamba wanafunzi huyo aliyedaiwa kutekwa na watu wasiojulikana, amepatikana Wilaya ya Mafinga akiwa mwenye afya njema na mwenye kujitambua akiendelea na shughuli zake.

Alisema licha ya kusambaa taharuki hiyo ya kutojulikana alipo, Nondo (24) hakuripoti tukio lolote kabla hajakamatwa ili kuthibitisha kama ametekwa na watu wasiojuliakana.

"Hakuripoti kwa mtu yoyote sio kwa mwenyekiti wa Serikali za mitaa, mtendaji wa kata wala polisi, Jeshi la polisi Kanda Maalum Dar es Salaam kwa kushirikiana na Polisi Iringa tulifanya uchunguzi na ufuatiliaji na kubaini hakutekwa," alisema na kuongeza:

"Tumebaini kuwa, mwanafunzi huyu alijiteka au aliamua kutoa taarifa hizo ambazo kimsingi zilikuwa na maslahi yake binafsi na kwa kuwa 'wanaodili' na mambo ya siasa pengine alifanya hivyo ili kujipatia umaarufu."

Alisema upelelezi umebaini alikwenda Iringa kwa mpenzi wake ambaye alikuwa akiwasiliana naye mara kwa mara akiwa njiani kuelekea mkoani humo.

"Hii ni baada ya kufanywa uchunguzi wa kisanyansi na kubaini muda ule aliosema ametekwa simu yake ilionyesha anafanya mawasiliano na binti aliyekuwa amemfuata Iringa," alisema.

Alisema mara baada ya kukamatwa walikwenda kumpima hospitali ili kubaini kama ana malaria iliyopanda kichwani lakini majibu yameonyesha hana hitilafu yoyote kichwani.

"Haya amefanya kwa makusudi kwa sababu anazozijua mwenyewe, tumebaini mara baada ya kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam alikuwa huru, alisafiri akiwa huru na akafika Iringa akiwa salama," alisema.

"Siyo hilo tu, simu yake imeonyesha mawasiliano ya kawaida baada ya muda aliosema ametekwa saa saba usiku, aliendelea kuwa na mawasiliano, aliendelea kutuma ujumbe kwa msichana aliyekuwa akienda kumtembelea Iringa."

Kamanda Mambosasa alisema kitendo kilichofanyika ni uzushi wenye malengo ya ovyo.

"Wapo watu wengine walishabikia suala hili, wengine huwezi kuamini kwa nafasi zao walilishikia bango jambo hili la aibu, mtu kuzusha jambo lilete taharuki kwa watu mwishoni ije kugundulika mtu huyu alikuwa huru."

Kutokana na kumtuhumu uzushi huko, Kamanda Mambosasa ametoa onyo kwa wananchi kuwa Jeshi la Polisi halitamnyamazia, kumuhurumia au kumwancha mtu yoyote ambaye anatafuta umaarufu uwe wa kiasiasa au wa aina yoyote.

"Kuzua taharuki na kufanya watu waendelee kulaumu waone hali si salama kwa sababu ya matendo ya kihuni aliyofanya kijana huyu (Nondo)," alisema.

Alisema wataendelea kusimama na kuchukua hatua kama walizomchukulia Nondo.

"Tutaendelea kumshikilia mwanafunzi huyu, taratibu zikikamilika atafikishwa mahakamani ili akajibu shtaka la uzushi na uongo uliopelekea kuleta usumbufu kwa watu wengine kikiwemo Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kikiamini mwanafunzi wao ametekwa."

Mwanzoni mwa wiki iliyopita, mwanafunzi huyo aliripotiwa kutoweka katika mazingira ya kutatanisha baada ya kufanya mkutano wa waandishi wa habari na baadaye kuaga anaelekea nyumbani kwao Madale.

Baada ya tukio hilo la kutoweka siku iliyofuata, Nondo ilidaiwa kuwa aliripoti Kituo cha Polisi Mafinga wilayani Mufindi baada ya kutangazwa kutoweka.

Alidai kutelekezwa na watu wasiojulikana ndipo aliposafirishwa kuja Dar es Salaam kwa mahojiano zaidi.

Katika mkutano wake na waandishi wa habari siku hhiyo, Mwenyekiti huyo wa TSNP, alimtaka Waziri wa Mambo ya Ndani ya nchi, Mwigulu Nchemba, ajiuzulu nafasi hiyo kutokana na kupigwa risasi mwanafunzi wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), Akwilina Akwilin mwezi uliopita.

Akwilina aliuawa kwa kupigwa risasi akiwa ndani ya daladala wakati wa maandamano ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) yaliyofanyika Februari 16.

Kutokana na mauaji hayo TSNP ilitoa tamko la kumtaka Mwigulu ajiuzulu nafasi yake kuonyesha uwajibikaji kutokana na kile ambacho jumuiya hiyo ilidai katika kipindi chake cha uongozi wizarani hapo, nchi imegubikwa na matukio mengi ya mauaji na utekaji wa raia pamoja na jeshi hilo kutozingatia maadili.

Baada ya kupotea, TSNP walitoa taarifa Kituo cha Polisi Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na kufunguliwa jalada UD/RB/1438/2018.

Habari Kubwa