Simu za kina Mbowe zapokewa kortini

19Jan 2022
Kulwa Mzee
DAR ES SALAAM
Nipashe
Simu za kina Mbowe zapokewa kortini

MAHAKAMA Kuu Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi, imepokea simu nne zikiwamo za Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe na mshtakiwa wa kwanza, Halfani Bwire kama kielelezo cha Jamhuri katika kesi ya ugaidi.

Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe (kushoto) na wenzake wakiwa chini ya ulinzi wa askari Magereza, walipowasili katika Mahakama Kuu Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi kusikiliza mashtaka ya ugaidi yanayowakabili. PICHA: JUMANNE JUMA

Vielelezo hivyo vilitolewa jana na shahidi wa 10, Inspekta Innocent Ndowo, na kupokewa mbele ya Jaji Joachim Tiganga anayesikiliza shauri hilo.

Shahidi huyo akiongozwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Pius Hillar, alidai ripoti aliyopeleka kwa wapelelezi iliambatana na vielelezo ambazo ni simu nne alizozipa alama ya E,F,G na H.

Alidai akiona anaitambua, miongoni mwa vitu vilivyoko vya kumwezesha kuitambua ni namba ya kesi CD/IR/2027/2020, majina, ina muhuli kwa niaba ya Kamishna wa Uchunguzi wa Kisayansi na ina saini ya Kamishna Msaidizi wa Polisi Naftal Joseph.

Shahidi baada ya kuelezea anavyotambua nyaraka aliomba kutoa kama kielelezo. Upande  wa utetezi haukuwa na pingamizi, mahakama ilipokea nyaraka hizo.

Mahakama ilipokea vielelezo hivyo sita, ripoti mbili zilitambulika kielelezo namba 22, 23, simu nne zilitambuliwa kwa IMEI namba 355029115930845 kielelezo namba 24, 353487133305 kielelezo namba 25, 358821101132040 kielelezo namba 26 na 352386071165127 kielelezo namba 27.

Miongoni mwa simu hizo kuna simu ya mshtakiwa Freeman Mbowe, Halfani Bwire na Luteni Dennis Urio ambazo zilifanyiwa uchunguzi wa miamala ya simu na usajili wake.

Shahidi anasoma baadhi ya ujumbe uliokutwa kwenye simu ya Luteni Urio kama ifuatavyo;-

“Tutumie nauli tukutane Morogoro, nipo njiani naelekea Singida, nimepata bro, tutaongea jioni.”

“Mh. habari za siku, Salama Kaka, Mhe. mmoja yuko Kigoma mtafanya naye kazi. Unamaliza lini huko? Mwezi wa tatu mwishoni.”

“Bro upo. Mara ya mwisho kuwasiliana na wewe ulisema unatoka Mtwara, Ohh kaka nakuombea heri.”

Shahidi alimaliza kusoma vielelezo vilivyopokewa mahakamani, upande wa mashtaka walimaliza kumwongoza, zamu ya mawakili wa upande wa utetezi kumuhoji maswali kutokana na ushahidi wake.

Washtakiwa katika kesi hiyo ni Mbowe, Bwire, Adamu Kasekwa na Mohammed Ling'wenya ambao wanashtakiwa kwa mashtaka sita ikiwamo kulanjama kufanya vitendo vya kigaidi kati ya Mei na Agosti mwaka 2020.

Habari Kubwa