Siri JPM kumpa Kairuki Madini

08Oct 2017
Romana Mallya
Nipashe Jumapili
Siri JPM kumpa Kairuki Madini

UIMARA aliouonyesha katika kufanikisha operesheni za kumaliza tatizo la watumishi hewa na wenye vyeti feki vya elimu na taaluma, ni miongoni mwa sifa zinazotajwa kumng’arisha Waziri Angellah Kairuki kiasi cha kuteuliwa na Rais John Magufuli kuongoza wizara mpya ya Madini.

Kairuki aliyekuwa Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Rais (Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora), aliteuliwa kuwa Waziri wa Madini katika mabadiliko makubwa ya Baraza la Mawaziri yaliyofanywa jana na Rais Magufuli.

Wizara hiyo mpya, ni matokeo ya uamuzi wa Rais Magufuli wa kuigawa iliyokuwa Wizara ya Nishati na Madini na kuwa mbili, lengo likiwa ni kuwezesha ufanisi katika kusimamia kwa ukamilifu maeneo hayo. Aliyekuwa Naibu Waziri katika wizara ya awali ya Nishati na Madini, Dk. Medard Kalemani, ndiye aliyeteuliwa kuwa Waziri wa Nishati.

Wizara hizo, ikiwamo ya Madini atakayoiongoza Kairuki baada ya kuapishwa Ikulu jijini Dar es Salaam kesho, zinaaminika kuwa na changamoto nyingi, hivyo kuchukuliwa kuwa fupa gumu kutokana na rekodi yake ya miaka ya karibuni kuonyesha kuwa wengi wanaoteuliwa huishia kung’olewa au kujiuzulu kutokana na sabanu mbalimbali, zikiwamo kashfa kubwa za kutikisa nchi.

Chini ya Kairuki, Wizara ya Utumishi imesimamia kwa ufanisi mkubwa uhakiki wa wafanyakazi hewa na wale wenye vyeti bandia.

Kupitia operesheni hizo kabambe za nchi nzima, serikali imeokoa jumla ya Sh. bilioni 381 zilizokuwa zikilipwa kila mwaka kwa watumishi hewa takribani 20,000 na wenye vyeti feki 12,000.

“Tangu ateuliwe na Rais Magufuli kuiongoza Wizara ya Utumishi, Kairuki amekuwa akifanya vizuri sana… mara zote huonekana imara katika kufanikisha malengo ya serikali ambayo ni kuimarisha utendaji wa watumishi wake ili mwishowe watumikie vyema wananchi,” mmoja wa wachambuzi wa masuala ya siasa aliiambia Nipashe jana na kuongeza:

“Hii ndiyo siri ya kupewa kwake Wizara ya Madini. Licha ya ugumu wake uliothibitishwa na wale waliowahi kuongoza eneo hilo, naamini Kairuki atafanya vizuri kama alivyothibitisha katika utumishi ambako pia kulikuwa na makandokando mengi.”

Kairuki atasaidiana na Naibu Waziri mpya Stanslaus Nyongo kusimamia maslahi ya serikali kwenye masuala ya madini, yakiwamo ya dhahabu, shaba, almasi, tanzanite na metali mkakati kama lithium ambayo ripoti za hivi karibuni za kamati teule za Rais Magufuli na Spika wa Bunge, Job Ndugai, zilibaini kutolinufaisha taifa kutokana na kasoro nyingi zilizokosesha nchi matrilioni ya shilingi.

Miongoni mwa mawaziri waliowahi kuiongoza wizara ya awali ya Nishati na Madini tangu enzi za awamu ya nne chini ya Rais mstaafu Jakaya Kikwete na kujikuta waking’oka mapema ni Dk. Ibrahim Msabaha, Nazir Karamagi, William Ngeleja na Prof.
Sospeter Muhongo (mara mbili). Pia George Simbachawene aliyewahi kuiongoza wizara hiyo, alilazimika kujiuzulu uwaziri wa Tamisemi hivi karibuni baada ya kuguswa na ripoti kuhusu biashara ya almasi na tanzanite.

Akizungumza uteuzi wa Kairuki katika Wizara ya Madini jana, Profesa Haji Semboja wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) Idara ya Uchumi, alisema ana imani kwamba Kairuki ataisimamia vizuri wizara hiyo kama ilivyokuwa ya Utumishi, licha ya kuwa ni wizara inayoonakana kuwa ngumu na kuwashinda wanaume wengi.

Prof. Semboja alisema kuwa Kairuki ni mchapakazi na hiyo ndiyo siri ya kupewa wizara hiyo, hivyo hatamuangusha Rais na Watanzania.

“Akiwa na wataalamu wenye uzoefu na elimu, akiwamo Kamishna wa Madini, na wakurugenzi ambao ni wachapakazi, mambo yataenda vizuri … hasa ukizingatia kwamba na yeye ni mchapakazi hodari. Kairuki ni mtendaji mzuri kwakweli,” alisema Semboja.

Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT), Prof. Elifas Bisanda, alipongeza hatua ya Rais Magufuli kwa kuigawa Wizara ya Nishati na Madini na kumteua Kairuki kuongoza mojawapo (ya Madini).

Bisanda alisema kuteuliwa kwa Kairuki kushika nafasi hiyo kunatokana uchapakazi aliouonyesha kwenye Wizara ya Utumishi na kwamba anaamini ataendelea kuwa mtendaji mzuri kwenye nafasi hiyo mpya.

“Mtu yeyote aliye mwadilifu anaweza kufanya kazi yoyote na utendaji wake ukaonekana kwa kuzingatia hilo. Mimi namwamini Waziri Kairuki… kwamba ataisimamia vizuri Wizara ya Madini,” alisema Prof. Bisanda.

Mchambuzi wa masuala ya kisiasa, Hashim Bindu, alisema Wizara ya Madini ina vishawishi vingi kutokana na biashara kubwa ya madini inayohusisha fedha nyingi hivyo kuteuliwa kwa Kairuki kunaashiria kuwa amebebwa na sifa ya uaminifu na uadilifu wake.

“Wizara ya Madini kama una tamaa huwezi kudumu hata miezi sita ndiyo maana mawaziri kwenye wizara hii wamekuwa hawamalizi muhula wa miaka mitano kama wa wizara zingine…wanawake wengi wana sifa ya uadilifu. Tumpe muda lakini naamni ataimudu,” alisema Bindu.

WATANGULIZI WALIVYONG’OKA
Rais mstaafu Kikwete alipoingia madarakani mwaka 2005, alimteua Mbunge wa Kibaha Vijijini, Dk. Ibrahim Msabaha kuwa Waziri wa Wizara hiyo. Alikaa katika wizara hiyo miezi minane na nafasi yake kuchukuliwa na Nazir Karamagi.

Hata hivyo, Karamagi na Msabaha (aliyehamishiwa Wizara ya Ushirikiano wa Afrika Mashariki), walijiuzulu kutokana na kashfa ya mkataba tata wa kampuni ya kufua Umeme ya Richmond sambamba na aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa. Baada ya hapo alifuatia Ngeleja mwaka 2008, ambaye naye aliondolewa mwaka 2012.

Baada ya Ngeleja kuondolewa, aliteuliwa Prof. Muhongo ambaye naye mwaka 2015 aliondolewa na Rais Kikwete, wakati huo kwa kashfa ya kuchotwa kwa fedha Akaunti ya Tegeta Escrow na licha ya kurejeshwa katika nafasi hiyo na Rais Magufuli, Muhongo alijikuta aking’oka tena Mei, 2017 baada ya kuanikwa kwa ripoti za kamati teule zilizochunguza usafirishaji wa mchanga wa dhahabu (makinikia) kwenda nje ya nchi.

BARAZA KAMILI JIPYA LA MAWAZIRI
Katika mabadiliko hayo ya Baraza la Mawaziri jana, Rais Magufuli aliongeza wizara kutoka 19 hadi 21 na kuteua sura kadhaa mpya huku wengine wa zamani akiwaacha. Aliowaacha katika uteuzi wa sasa ni pamoja na aliyekuwa Waziri wa Malisiali na Utalii, Prof. Jumanne Maghembe na pia aliyekuwa Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Gerson Lwenge.

Naibu Mawaziri walioachwa ni Ramo Makani (Nishati na Madini) na Anastazia Wambura (Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo)
Katika Wizara ya Nishati inayoongozwa na Kalemani, Naibu Waziri aliyeteuliwa kuwa naye ni Subira Mgalu.

Rais Magufuli aliigawanya pia Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi na sasa zitatambulika Wizara ya Kilimo ambayo waziri wake ni Dk. Charles Tizeba na Naibu Waziri ni Mary Mwanjelwa.

Wizara mpya ya Mifugo na Uvuvi waziri wake ni Luhaga Mpina, ambaye amepanda cheo kutoka Naibu Waziri Ofisi ya Rais Muungano na Mazingira na Naibu Waziri ni Abdallah Ulega.

Kwa upande wa Wizara ya Viwanda Biashara na Uwekezaji, Rais Magufuli amemwacha Charles Mwijage kuendelea kuwa waziri na kumteua Mhandisi Stella Manyanya kuwa Naibu Waziri. Awali alikuwa Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi Teknolojia na Ufundi.

Wizara nyingine ambayo Rais Magufuli ameiongezea nguvu ni Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), ambayo waziri wake anakuwa Selemani Jafo akisaidiwa na manaibu wawili, ambao ni Josephat Kandenge na George Kakunda. Jafo amepanda kutoka naibu waziri katika wizara hiyo.

Rais alisema amewaweka manaibu waziri wawili Tamisemi kwa sababu wizara hiyo inagusa wananchi na kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo.

Katika Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Prof. Makame Mbarawa anaendelea kuwa Waziri na wameteuliwa naibu mawaziri wawili ambao ni Mhandisi Atashasta Nditiye, atakayeshughukulikia Ujenzi na Elias Kwandikwa (Uchukuzi na Mawasiliano).Wengine walioteuliwa ni George Mkuchika ambaye amekuwa Waziri ya Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora huku Wizara ya Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, akibaki January Makamba na Naibu Waziri wake ni Kangi Lugola.

Waziri Jenister Mhagama (Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu) na Naibu Waziri ni Antony Mavunde wamebaki kwenye nafasi zao na wameongezewa Naibu Waziri atayeshughulikia Walemavu, Stella Ikupa.

Wizara ya Fedha na Mipango amebaki Dk. Philip Mpango na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Dk. Ashatu Kijaji huku Wizara ya Katiba na Sheria, amebaki Prof. Palamagamba Kabudi na Wizara ya Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa akiendelea Dk. Augustine Mahiga na naibu wake, Dk. Susana Kolimba

Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) amebaki Dk. Hussein Mwinyi, Wizara ya Mambo ya Ndani akiendelea Mwigulu Nchemba na Naibu Waziri ni Hamad Yusuf Masauni.

Aidha, katika Wizara ya Maliasili na Utalii, ameteuliwa Dk. Hamis Kigwangalla kushika nafasi hiyo akiwa na naibu wake, Japhet Hasunga. Kabla ya hapo Kigwangalla alikuwa naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto.

Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi amebaki William Lukuvi na Naibu wake ni Angelina Mabula.

Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi, amebaki Prof. Joyce Ndalichako na Naibu Waziri ni William Ole Nasha ambaye awali alikuwa Naibu Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi. Katika Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, amebaki Ummy Mwalimu na Naibu Waziri aliyeteuliwa ni Dk. Faustine Ndungulile.

Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo amebaki Dk. Harrison Mwakyembe na Naibu Waziri aliyeteuliwa ni Juliana Shonza wakati katika Wizara ya Maji na Umwagiliaji, ameteuliwa Mhandisi Isack Kamwelwe na Naibu Waziri anakuwa Jumaa Aweso. Awali, Kamwelwe alikuwa naibu waziri katika wizara hiyo.

Rais Magufuli alisema licha ya Baraza la Mawaziri kuwa na mawaziri 21, naibu mawaziri wameongezeka pia kutoka 16 hadi 21, hivyo idadi ya mawaziri iliyoongezeka ni wawili na manaibu ni watano.

KATIBU WA BUNGE ANG’OLEWA
Katika hatua nyingine, Rais Magufuli alimteua Stephen Kagaigai kuwa Katibu wa Bunge na kumwondoa Dk. Thomas Kashilila ambaye atapangiwa kazi nyingine. Rais Magufuli alisema wote walioteuliwa wataapishwa kesho asubuhi Ikulu.