Siri mwizi kukutwa amechapa usingizi kwa mwandishi ITV

03Jun 2020
Rahma Suleiman
Zanzibar
Nipashe
Siri mwizi kukutwa amechapa usingizi kwa mwandishi ITV

KIJANA anayedaiwa kuwa mwizi aliyetambulika kwa jina la Daudi Suleiman maarufu kama ‘Kiboko’, amejikuta amelala katika gari la mwandishi wa habari wa ITV Zanzibar, Farouk Karim, ikidaiwa aliingia katika gari hilo kwa lengo la kutaka kuiba.

Tukio hilo lilitokea usiku wa kuamkia juzi ambapo kijana huyo akiwa na vitu mbalimbali alivyoviiba, alinasa katika gari hilo na kulala usingizi usiku kucha bila kujitambua.

Akizungumza na Nipashe, Farouk Karim alisema kuwa kijana huyo aliingia katika nyumba yake kwa kuruka ukuta na kuiba vitu mbalimbali.

Pia alibainisha kwamba mtuhumiwa huyo alivunja gari lake na kutaka kuiba, lakini alinasa akiwa ndani ya gari na kulala humo hadi asubuhi.

Nipashe ilimuuliza Farouk aliweka mtego gani ambao ulimfanya mwizi huyo kunasa, alisema yeye hana mtego wowote aliotumia, isipokua ni kumwamini Mungu.

“Mimi sina dawa yoyote niliyotumia, Mungu tu kataka kumuadhiri kijana huyo ambae ni mwizi maarufu hapa mtaani petu Fuoni,” alisema.
Alieleza kuwa kijana huyo kwa sasa anashikiliwa na Jeshi la Polisi kwa hatua zengine za kisheria.

Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja, Simon Pasua, alisema kuwa Jeshi la Polisi linamshikilia kijana huyo, na uchunguzi utakapokamilika atafikishwa mahakamani.

Habari Kubwa