Siri ugumu kunguni kufa, wanavyotesa familia nyingi

01Jul 2019
Romana Mallya
Dar es Salaam
Nipashe
Siri ugumu kunguni kufa, wanavyotesa familia nyingi

KUNGUNI (Bedbugs) ni mdudu mwenye uwezo mkubwa wa kustahimili hatari dhidi ya maisha yake na utafiti mbalimbali unaonyesha sumu inayoweza kuua viumbe wengine, humuimarisha zaidi badala ya kumuua.

KUNGUNI.

Mdudu huyo ambaye hupenda kuishi maeneo ya joto na kujificha mahali popote, kwenye godoro, fanicha, ukutani na katika pindo za nguo, kwa sasa ni miongoni wa wadudu ambao wanawatesa familia nyingi kutokana na tabia yake ya kutokufa kwa sumu kwa urahisi, hivyo kusababisha kuzaliana kwa wingi.

Uchunguzi uliofanywa maeneo tofauti jijini Dar es Salaam na kuongea na wananchi wa jiji hilo, umebaini idadi kubwa ya familia zimeathiriwa na mdudu huyo na wapo waliotumia Sh. milioni 40 kukabiliana nao bila mafanikio.

Kwa kawaida kunguni hupenda kujificha karibu na binadamu kutoka mita tatu hadi sita kwenye vitanda na maeneo ya kukaa ili iwe rahisi nyakati za usiku kunyonya damu.

WAATHIRIKA WASIMULIA

Mzazi wa mwanafunzi mmoja anayesoma katika Shule ya Msingi ya Atlas, Madale, ambaye hakutaka jina lake liandikwe, alisema, mtoto wake ambaye yupo bweni shuleni hapo, alianza kulalamika tangu mwaka jana kuwapo kwa kunguni bwenini.

“Mtoto wangu wakati wa likizo mwaka jana aliniambia kuwa shuleni kuna kunguni ambao wamekuwa wakiwakosesha usingizi, baada ya taarifa hiyo niliwasiliana na uongozi wa shule nao ulithibitisha na mwishoni mwa mwaka jana kabla ya shule kufungwa, kilifanyika kikao cha wazazi na uongozi wa shule,” alisema.

Mzazi huyo alisema katika kikao hicho uongozi wa shule uliwahakikishia kuwa shule itakapofunguliwa mwanzoni mwa mwaka huu tatizo hilo litakuwa limekwisha, ingawa hadi sasa bado.

“Mtoto wangu alikuwa akilalamika kuwa wakilala vitandani zikizimwa taa wanang’atwa zaidi kuliko zinapowashwa, lakini matroni wao licha ya kuwapo kwa tatizo hilo, alikataa uwashaji wa taa nyakati za usiku, hivyo mwanangu anasema wamekuwa waking’atwa sana wanapoingia vitandani kuanzia saa sita usiku,” alisema.

Alisema likizo ya mwezi huu uongozi wa shule hiyo ulimpigia simu na kumtaka ama walichukue godoro kwa ajili ya kwenda kulihudumia nyumbani ili kuangamiza wadudu hao au libaki shule kwa sharti kwamba liwe na kava.

“Tulilichukua godoro na tulipofika nyumbani tuliliweka nje nyakati zote na tulikuwa tukilipulizia dawa na kulianika kwenye jua hadi aliporudi shule. Hii ilikwenda sambamba na vitu vyote alivyotoka navyo shule viliishia nje tulihofia wasisambaze ndani,” alisema.

Mzazi mwingine katika shule hiyo ambaye naye hakupenda jina lake liandikwe, alisema licha ya mtoto wake kuwa mwanafunzi wa kutwa, amekuwa akilalamika kuwa mara kwa mara wawapo darasani wamekuwa wakiwaona kunguni kwenye sare za shule na begi.

“Yaani sasa imekuwa kama ni mtihani akirudi nyumbani kabla ya kuingia ndani anavua kila kitu nje na anaacha na begi, tunapukuta tukiwakuta tunawaua, hofu kama mzazi ni kwamba wasijeingia ndani wakazaliana,” alisema.

Baadhi ya wanafunzi wa shule hiyo wakizungumza na gazeti hili walisema kuwa kuwapo kwa wadudu shuleni hapo kumewaathiri kisaikolojia kwa sababu muda ambao wanatakiwa kulala baada ya kutoka kujisomea, wanashindwa kwa sababu mara tu waingiapo vitandani, huanza kung'atwa.

Mwanafunzi wa darasa la nne ambaye (jina linahifadhiwa), alisema amekuwa akikosa raha kwa sababu hata akiwa darasani yale maumivu ya kung'atwa yamemfanya wakati wote kuhisi hivyo.

"Ninakosa raha na amani mara giza linapoingia ninawaza kunguni, maana ukiingia kitandani kulala tu taa ikizimwa unaanza kung'atwa na kujikuna, hali hii imenifanya hata nikiwa darasani mwalimu akifundisha nahisi nang'atwa tu," alisema.

Mwanafunzi mwingine wa darasa la saba shuleni hapo (jina linahifadhiwa), alisema kuwa wakati mwingine akiwa darasani anawaona wadudu hao kwenye sare ya shule.

"Wakati mwingine unawakuta kwenye begi, wakati mwingine mwalimu akiwa anafundisha unashangaa mwenzako anakukung'uta nguo, ukimgeukia anakwambia ni kunguni. Binafsi usiku silali kwa raha tukitoka kujisomea usiku ukimaliza ukiwa umechoka ukiingia kitandani wanaanza, kuna wakati ilifikia tukawa hatuzimi taa angalau hatung'atwi kama ikizimwa lakini sasa matroni hataki taa iachwe bila kuzimwa," alisema.

Alisema hali hiyo ya kung'atwa kila wakati imemuathiri hata kwenye masomo kwa sababu ya kutolala vizuri usiku na kutumia muda mwingi kuhisi anang'atwa.

"Tunaomba wazazi na walimu washirikiane kuhakikisha wadudu hawa wanaisha kabisa maana bila kufanya hivyo tutafeli mitihani kwa sababu ukifika darasani badala ya kumsikiliza mwalimu unajikuta unasinzia kutokana na usiku kucha hukulala vizuri, tunaolalamika siyo sisi peke yetu tunaolala bweni hata wanaoondoka nyumbani kwa sababu tunasoma madarasa hayo hayo muda mwingi tupo pamoja wa hiyo tunawabeba mabwenini tunawaleta darasani nao wanawapeleka majumbani, hata sisi tukifunga shule tunawahamishia majumbani kwetu, ndio maana tunaomba ushirikiano wa wazazi na walimu kumaliza tatizo hili shuleni kwetu," alisema.

MILIONI 40 ZATUMIKA KILA MWAKA

Mmiliki wa Shule ya Msingi na Sekondari Atlas iliyopo Madale, Sylivanus Rugambwa, alikiri shule yake kuwa na tishio la kunguni kwa miaka mitatu sasa na kila mwaka wanatumia Sh. milioni 40 kukabiliana nao.

Rugambwa alisema wameshatumia njia mbalimbali za kukabiliana na wadudu hao bila mafanikio na likizo ya mwezi huu wameamua kila mzazi aende shuleni hapo kuchukua godoro la mtoto wake ili wakaweke foronya ya godoro (cover) ambayo ndiyo njia ya kupambana nao.

“Tumeona huu ndio mkakati wa mwisho wa kukabiliana na kunguni, maana shule nyingine za wenzetu ndiyo wametumia kukabiliana nao,” alisema.

Aliongeza: “Kila mwaka tunatumia Sh. milioni 40 kukabiliana na kunguni kwa upande wa shule ya msingi na sekondari, kila nusu muhula tunatumia milioni 10, muhula tumeigawanya mara nne, hivyo kwa mwaka tunatumia Sh. milioni 40 kwa upande wa shule ya msingi na kwa upande wa shule ya sekondari.”

Alisema walichoamua ni kwenye likizo ya Juni, kila mzazi anatakiwa kwenda shuleni kuchukua godoro la mtoto wake ili akaliwekee foronya ambayo inatakiwa kuwa na zipu mbili kama za hospitali.

“Tatizo la kuongezeka kwa wadudu hawa pia linasababishwa na baadhi ya wanafunzi ambao bado wanajikojolea kuwafanya kunguni kuongezeka,” alisema.

Alisema ndani ya miaka mitatu, wamepuliza dawa za kuua wadudu, lakini hazijasaidia, na ndiyo maana uongozi wa shule umeamua kuja na mkakati wa magodoro yote yawekwe foronya.

“Wito wangu kwa wazazi wenye watoto shule ya Atlas watekeleze kilichoelekezwa, sasa hivi wakati wa likizo wakati uongozi ukiendelea kupambana kwa kuweka mazingira mazuri kwa kufungua vitanda na maeneo yote yenye mazalia kuyatokomeza na kupaka kuta rangi,” alisema.

Mkuu wa Kitendo cha Mawasiliano ya Serikali, Ofisi ya Rais Tamisemi, Rebecca Kwandu, alipoulizwa kuhusu changamoto ya wadudu hao mashuleni na kama kuna kuna mikakati ya kupulizia dawa mara kwa mara, alisema hawajapokea malalamiko kuwapo kwa kunguni shule za bweni na za kutwa.

“Ila kama kuna changamoto hiyo kwa sababu shule zina uongozi na zina wataalamu wa afya mara nyingi matatizo yanapotokea wanayamaliza huko huko au kuyafikisha kwenye mikoa yao husika, kuhusu serikali kuu hawajatufikishia,” alisema.

WAGONGA HODI MAJUMBANI

Fatuma Abdallah, mkazi wa Tandale, aliliambia gazeti hili kuwa hafahamu wapi alipomtoa mdudu huyo, ambaye amemsababishia hasara kubwa ya vitu vyake vya ndani.

Alisema alianza kuhisi kung’atwa kila akilala ndipo alipoanza kufuatilia na kubaini kwenye chaga za kitanda kumejaa mayai mengi na kunguni waliozaliana wakubwa kwa wadogo.

“Nimeshapulizia sumu za kila aina, nikajaribu kubadilisha godoro na kununua jipya, lakini sijapata ahueni, wengine waliniambia nitoe nje vitu vyote ambavyo ni makochi, godoro, kitanda na nguo ambavyo ndivyo kupenda kujificha ili vipuliziwe dawa na kumwagia maji ya moto, lakini sijaona matokeo,” alisema.

Alisema wapo waliomweleza kuwa wadudu hao wanapoona mwanga wa jua hulichukia, hivyo kila siku alilazimika kutoa vitu nje kuvianika na jioni kuvirudisha ndani bila mafanikio.

“Usiombee ukaingiwa na huyu mdudu kwanza kumwondoa ndani ni gharama na ni kazi kubwa, hawafi mapema na wanazaliana sana na sidhani kama wanakufa kwa sumu, naona wanaongezeka badala ya kupungua licha ya kuwapulizia dawa,” alisema.

Agnes Moses (siyo jina lake halisi) anasimulia kuwa mmoja ya watoto wa ndugu yake walipata matatizo akawekwa moja ya mahabusu (anaitaja) jijini Dar es Salaam baada ya kutoka alifikia nyumbani kwake, Mikocheni.

Alisema baada ya kijana huyo kukaa siku chache na baadaye kuondoka, wakati wakifanya usafi kwenye chumba alichokuwa akilala, walikuta idadi kubwa ya kunguni.

“Tumeshatumia dawa za kila aina, kuna dawa ambayo tuliambiwa ndiyo kiboko kutoka Afrika Kusini, tulinunua tukatumia kuwaangamiza, lakini baada ya muda hali imerejea. Tunachofanya sasa ni kupiga dawa na kutoa magodoro na viti nje kila siku, lakini bado wapo,” alisema.

Aliongeza: “Kunguni akiingia ndani ni kero huwezi kummaliza, gharama tuliyotumia ni zaidi ya milioni, lakini hatujafanikiwa, ukikaa kwenye kochi wapo, vyumbani wapo.”

Alisema kutokana na changamoto hiyo anaogopa kutembelewa ndugu, jamaa na marafiki au wao kwenda kwao kwa kuhofia kuwasambaza.

JESHI LA POLISI LAFUNGUKA

Akitolea ufafanuzi kuhusu malalamiko ya baadhi ya mahabusu kudaiwa kuwa na kunguni, Msemaji wa Jeshi la Polisi nchini, David Misime, aliliambia gazeti hili kuwa ofisi zote za serikali zina utaratibu wa kupulizia dawa za kuua wadudu mara kwa mara.

“Utaratibu uliopo kila siku asubuhi mahabusu husafishwa tena siyo kwa maji, wanasafisha kwa kutumia maji yenye dawa ili kuua wadudu pamoja na hao unaowataja. Pia upo utaratibu wa kupulizia dawa ya kuua wadudu ‘fumigation’ baada ya muda fulani ili kuondokana na maambukizi ya magonjwa kwa sababu sehemu hizo huingiwa na watu wa aina tofauti tofauti,” alisema.

SERIKALI YATOA HOFU

Naibu Waziri wa Wizara ya afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Faustine Ndugulile, aliliambia Nipashe kuwa kunguni haambukizi magonjwa kwa binadamu zaidi huleta maudhi.

“Kimsingi, kunguni ni wadudu ambao kitaalamu siyo vijidudu vinavyosababisha magonjwa, lakini kama wataalamu wa afya tunaona ni mdudu anayeleta maudhi, anapokuuma unawashwa unajikuna.

Aliongeza: “Mtu anapowashwa sana anajikuna na akijikuna sana, anaweza kupata maambukizi mengine ya ngozi ambayo sasa inaweza kumletea mtu madhara zaidi. Lakini kunguni kama mdudu siyo vijidudu vinavyosababisha magonjwa.”

Dk. Ndugulile alibainisha mdudu huyo anahusishwa masuala ya usafi wa mazingira ya mtu binafsi na kubainisha kuwa kama yatakuwa machafu uwezekano wa mdudu huyo kuwapo ni ukubwa.

“Unapokuwa na mazingira safi basi kunguni siyo rafiki wa usafi, unapoona sehemu ina kunguni maana yake hali ya usafi hairidhishi. Nitumie fursa hii kutoa rai kwa jamii, shule na maeneo mengine kuhakikisha mazingira yetu wakati wote yanakuwa masafi,” alisema.

Dk. Ndugulile alibainisha kuwa wadudu hao hupenda kujificha kwenye kuta zenye nyufa, chaga za vitanda, magodoro na maeneo mengine yasiyo na mwanga.

“Kama ukiona una tatizo la kunguni jitahidi vitu vyako uvitoe nje uvianike kwenye jua, hakikisha unatumia maji ya moto kufua matandiko, kuanika madogoro juani na kupulizia dawa, lakini kikubwa zaidi ni kuzingatia usafi na nyumba zenye nyufa zizibwe,” alisema.

Kuhusu utafiti ambao umefanyika hadi sasa ambao unabainisha kuua kunguni kirahisi kwa sumu, Dk. Ndugulile alisema siyo kweli na kueleza kuwa zipo kemikali ambazo zinaweza kutumika kuwaangamiza.

“Siyo kila dawa unayoitumia inaua mdudu, kwa sababu viumbe hivi vimeumbwa kwa utofauti na hali ya upokeaji wake wa dawa, ni vizuri mtu anayesumbuliwa na kunguni apate ushauri kwa washauri wataalamu ili upate njia sahihi ya kuwaua,” alisema.

UTAFITI DUNIANI

Utafiti uliofanywa kuhusu mdudu huyu umekuja na matokeo kuwa, wanaweza kustahimili kupuliziwa dawa nyingi ya sumu kwa kuimarisha uwezo wake wa kujikinga dhidi ya sumu moja baada ya nyingine.

Mdudu huyo ameonyesha ana uwezo mkubwa wa kibaiolojia ya kujikinga dhidi ya sumu kali na kadri vizazi vya kunguni vinavyopuliziwa dawa yenye sumu ndivyo wanavyoimarisha uwezo wao wa kuzuia maafa miongoni mwa watoto wao.

Taarifa iliyochapishwa katika jarida la utabibu la The Journal of Medical of Entomology, watafiti wanasema vipimo 1000 vya sumu kali aina ya (neo-nicotinoid) vinahitajika kuua kunguni mmoja huko Marekani katika majimbo ya Cincinnati na Michigan ikilinganishwa na maeneo mengine duniani.

“Kuna hatari kubwa ya mdudu huyu kuenea kote duniani kutokana na utandawazi na soko huria ambao umefanya ulimwengu kuwa kitongoji kikubwa tu,” watafiti hao wanabainisha.

Wanasayansi hao wanashauri kutafutwa mbinu mpya tofauti ya kukabiliana na wadudu hao badala ya kutumia sumu, kutafuta wadudu wengine wanaoweza kuwala ilikuzuia kunguni kuenea duniani kote.

RANGI WAZIPENDAZO

Watafiti nchini Marekani baada ya kufanya uchunguzi wa kina, wamebaini kunguni hupenda baadhi ya rangi kushinda nyingine.

Uchunguzi uliofanywa na watafiti hao umebaini wadudu hao hupenda rangi nyeusi na nyekundu na huchukia njano na kijani kibichi.

Matokeo ya utafiti huo ambayo yalichapishwa katika jarida la kimatibabu la Journal of Medical Entomology, watafiti hao wanasema bado ni mapema kubaini iwapo shiti za rangi ya njano zinaweza kutumiwa kuwafukuza wadudu hao kitandani au la.

Daktari Corraine McNeill na wenzake walitaka kubaini iwapo rangi zinaweza kuathiri maeneo wanayovamia na wadudu hao.

Katika uchunguzi wao walitumia vibanda vidogo vya rangi mbalimbali kwenye maabara na kuchunguza kunguni ndipo alipobaini wanapenda rangi hizo mbili.

"Hata hivyo, baada ya uchunguzi, sababu kuu tuliyobaini iliwafanya kupenda rangi nyekundu ni kwa sababu kunguni wenyewe huonekana wakiwa wa rangi nyekundu, hivyo hudhani rangi hiyo ni kunguni wenzao,” walibainisha watafiti.

Utafiti uliofanywa awali umebainisha kwamba rangi hizi pia hazipendwi na wadudu wengine wafyonza damu kama mbu.

MWONEKANO WAKE

Kwa wasiomjua, kunguni ni mdudu mdogo mwenye miguu sita, kulia mitatu na kushoto mitatu na hawezi kuruka kama mende, hutambaa na huishi kwa kutegemea damu kama chakula chake ndiyo maana amekuwa msumbufu kwa watu.

Wadudu hawa wapo wa aina nyingi, wanaouma popo tu na wapo wanaowauma binadamu.

Kihistoria wadudu hawa walikuwapo enzi na enzi, lakini mwaka 1940 walimalizwa katika nchi zilizoendelea kama Marekani na za Ulaya, lakini ilipofika mwaka 1995 walirudi upya.

Sababu za kurudi kwao zinatajwa ni dawa za kuwaua ziliwatengenezea usugu, hivyo kukosa nguvu ya kuwaangamiza, kupigwa marufuku dawa hizo baada ya kuthibitika zina madhara kwa binadamu na huweza kusafiri nchi moja hadi nyingine.

Mdudu huyo hutaga yai kila siku kuanzia yai moja hadi matano na baada ya yai anakuwa mdogo mwenye milimita 1.5, kisha hukua hatua kwa hatua hadi anafikia kuwa kunguni kamili.

TABIA ZA KUNGUNI

Mara nyingi mdudu huyu amekuwa na tabia ya kujificha hasa nyakati za mchana kwenye maeneo ambayo siyo rahisi kugundua kama wapo na hushamiri na kuonyesha makeke yao nyakati za usiku watu wakiwa wamelala.