Sirro alivyotoa somo udhibiti wahalifu kutoka Burundi, DRC

16Dec 2017
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Sirro alivyotoa somo udhibiti wahalifu kutoka Burundi, DRC

MKUU wa Jeshi la Polisi, IGP Simon Sirro, amewataka wananchi wa mikoa ya mpakani ukiwamo Kigoma kujiweka mbali na vitendo vya kuhifadhi wageni wanaoingia nchini kinyume cha sheria kwa lengo la kuweka nchi katika hali salama dhidi ya wahalifu.

IGP Sirro (katikati anayetabasamu) akishiriki mazoezi na baadhi ya askari wa kikosi maalum cha  haraka cha kupambana  na matukio makubwa ya kihalifu kwenye viwanja vya FFU mkoani Kigoma, mwishoni mwa wiki. (Picha: Magreth Magosso)

Kamanda Sirro alitoa somo hilo la namna ya kudhibiti wahalifu watokao nje ya nchi mwishoni mwa wiki wakati akiwa mkoani Kigoma katika ziara yake ya siku mbili kuangalia utendaji kazi wa jeshi lake mkoani humo.

Katika maelezo yake hayo, Kamanda Sirro alisisitiza kuwa kitendo cha kuhifadhi wageni kinyume cha sheria ni kosa la jinai na kwamba, kufanya hivyo ni sawa na kuiweka nchi katika hatari ya kupokea watu wenye dhamira ya kutenda uhalifu pasi na kujua.

Aidha, IGP Sirro alisema kuwa jambo jema kwa kila mkazi wa Kigoma ni kuhakikisha kwamba hakuna mgeni wanayemhifadhi kinyume cha sheria na taratibu za nchi, na hiyo iwe kwa watu wote hata kama wahusika wana uhusiano wa kindugu na wageni hao.

Alisema wananchi wa Kigoma wanapaswa kuongeza umakini katika kuzingatia jambo hilo kwa sababu upo uwezekano wa kuingia nchini kinyume cha sheria kwa watu watokao nchi zinazopakana na mkoa huo za Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na mwishowe kuhatarisha usalama wa  Watanzania na mali zao.

"Hata kama ndugu yako anaishi Burundi, muache aendelee na maisha yake ya Burundi. Kukaribisha watu ambao huwezi kujua dhamira yao ni hatari… ndiyo hao (baadhi) wanafanya uhalifu," alisema Sirro, akisisitiza kuwa umakini katika kuepuka upokeaji wa raia wa kigeni wanaongia bila kufuata sheria ndiyo utakaosaidia kujiepusha na wahalifu watokao kwenye nchi hizo.

Katika hatua nyingine, IGP Sirro alisema kuwa jitihada zinazoendelea kufanywa zimesaidia kupunguza matukio ya uporaji wa kutumia silaha kulinganisha na miaka iliyopita na kwamba sasa, mkakati uliopo ni kumaliza kabisa tatizo hilo.

"Wamenisomea taarifa ya mkoa hivi sasa. Matukio ya uhalifu kwa mkoa wa Kigoma yamepungua ukilinganisha na mwaka jana… tumepanga na IGP wa Burundi mwezi ujao tusaini mkataba wa kufanya operesheni ya pamoja," alisema Sirro. 

  

Habari Kubwa