SIRRO AWAPONGEZA WASTAAFU KUMALIZA BILA KASHFA

06Jan 2019
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe Jumapili
SIRRO AWAPONGEZA WASTAAFU KUMALIZA BILA KASHFA

MKUU wa Jeshi la Polisi Nchini, IGP Simon Sirro amewapongeza Wastaafu wa Jeshi hilo kwa kumaliza utumishi wa umma wakiwa hawana kashfa yoyote ambayo ingelichafua jeshi hilo na kufanya lipoteze uhalali mbele ya wananchi.

MKUU wa Jeshi la Polisi Nchini, IGP Simon Sirro

 

IGP Sirro ameyasema hayo wakati wa Sherehe ya Kuwaaga Askari na Wastaafu wa Jeshi na Sherehe ya Kuukaribisha Mwaka Mpya wa 2019 iliyofanyika katika Ukumbi wa Bwalo la Polisi, Oysterbay jijini Dar es Salaam.

 

“Nawapongeza kwa kumaliza salama naomba mkawe na nidhamu ya fedha mtakayolipwa kama kiinua mgongo na mtumie kiasi hicho cha pesa kwa manufaa ya familia na jamii inayowazunguka” alisema IGP Sirro

 

Akizungumza katika Sherehe hizo Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama, Jenerali Venance Mabeyo amewataka Wastaafu wa Jeshi la Polisi kuhakikisha wanakuwa raia wema na kudumisha amani katika maisha yao mapya baada ya kulitumikia Taifa kwa manufaa,ameongeza kuwa Upendo waliouonesha kwa wafanyakazi wenzao wakati wakiwa kazini wakauonyeshe huko wanakoenda.

 

“Mmekuwa mfano wa kuigwa kipindi chote mlichokua kazini, tunaomba mkawe raia wema huko kwa kuendelea kusimamia matukio ya uhalifu katika maeneo mtakayokua mnaishi, tunaamini nyie bado askari na mnafahamu mbinu zote za kupambana na uhalifu hivyo fahamuni tunawategemea bado,” alisema Jenerali Mabeyo.

 

Maafisa na Askari Wastaafu wa Jeshi la Polisi walioagwa katika sherehe hizo walilishukuru Jeshi la Polisi kwa upendo walioupata katika kipindi cha utumishi kwa umma na kuwaasa maafisa na askari walipo kazini kulitumikia jeshi kwa uaminifu mkubwa.

Habari Kubwa