Sita mbaroni kwa tuhuma za kukutwa na bunduki

05Jan 2017
Anceth Nyahore
MEATU
Nipashe
Sita mbaroni kwa tuhuma za kukutwa na bunduki

WATU sita wakazi wa Kijiji cha Mwabagimu wilayani Meatu wamekamatwa kwa tuhuma za kukutwa na silaha, ngozi ya mnyama aina ya nyegele na kilo nane za pembe za ndovu kinyume cha sheria.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Simiyu, Onesmo Lyanga, akiwa na waziri mkuu kassim majaliwa.picha na maktaba

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Simiyu, Onesmo Lyanga, aliwaambia waandishi wa habari ofisini kwake jana kuwa
watuhumiwa hao walikamatwa Januari 2, mwaka huu saa 11:00 jioni kijijini hapo.

Kamanda Lyanga aliitaja silaha inayodaiwa kukutwa kwa watuhumiwa hao kuwa ni aina ya Rifle 375 yenye namba za usajili 7054 pamoja na pinde mbili zenye mishale 10, sita kati yake ikihisiwa kuwa na sumu kali.

Kamanda Lyanga alisema mishale hiyo sita inayohisiwa kuwa na sumu, inafanyiwa utaratibu wa kupelekwa kwa Mkemia Mkuu ili kubaini aina ya sumu na madhara yake.

Aidha, aliwataja watuhumiwa hao kuwa ni Nghanga Ngusa (37), Machimu Ngusa (25), Mazongu Ngusa (22),
Masasila Ngusa (20), Kulwa Ngusa (20) na Ntunga Shija (30) wote wakazi wa kijiji hicho.


Kamanda Lyanga alifafanua kuwa tukio hilo lilitokea siku polisi wakiwa katika ulinzi wa kutekeleza amri ya Baraza la Ardhi chini ya usimamizi wa Inspekta wa Polisi, Frednand Bundala kwa ajili ya kutoa ulinzi kwa dalali wa mahakama, Abdallah Subira.

Hata hivyo, alisema utekelezaji wa amri hiyo ulikabiliwa na upinzani mkubwa kutoka kwa mshindwa tuzo na watu wengine walioamriwa kuondoka katika ardhi husika na kuanza kuwashambulia kwa mishale inayodhaniwa kuwa na sumu kali.


Kufuatia hali hiyo, ndipo polisi walipoamua kutumia mabomu ya kutoa 
machozi na kuwazidi nguvu.

Kamanda Lyanga alisema watu hao walikimbilia katika nyumba moja na kukamatwa.

Kamanda Lyanga alisema wakati polisi wakiwa wameizunguka nyumba hiyo ili kuwakamata watu hao, mmoja wao alitoka kwa kupitia mlango wa nyuma
akiwa na bunduki hiyo kwa nia ya kwenda kuificha, lakini alidhibitiwa na
silaha kukamatwa.

Alisema baada ya mtuhumiwa huyo kuhojiwa, iligundulika kuwa hakuwa na kibali cha kuimiliki silaha hiyo.

Aidha, Kamanda Lyanga alisema watu wengine watano waliokuwa ndani ya nyumba hiyo walijisalimisha.

Alisema askari walifanya upekuzi ndani ya nyumba hiyo na kukuta pembe mbili za ndovu zenye thamani ya Sh. milioni 8.8 na ngozi moja ya mnyama aina ya nyegele yenye thamani ya Sh. 600,000.

Kamanda Lyanga aliwapongeza askari walioshiriki katika mapambano kwa
kutumia umahiri mkubwa na kufanikiwa kuwakamata watuhumiwa bila
kuwajeruhi, jambo ambalo halikuwa rahisi kutokana na watuhumiwa kuwa na silaha.

Aidha, Kamanda Lyanga ametoa wito kwa wananchi kuacha kujihusisha na ujangili pamoja na kuwaomba raia wema kutoa taarifa za kihalifu ikiwa ni mchango wao wa kuondoa uhalifu.

Habari Kubwa