Sita wajeruhiwa na fisi aliyevamia kijiji

30Mar 2020
Marco Maduhu
Shinyanga
Nipashe
Sita wajeruhiwa na fisi aliyevamia kijiji

WATU sita wakazi wa kijiji cha Mwangalanga, Kata ya Samuye wilayani hapa, wamejeruhiwa na fisi wakati wakimshambulia.

Tukio hilo lilitokea Machi 27, saa 10 jioni, katika kijiji cha Mwangalanga wakati fisi huyo alipovamia kijiji hicho na wananchi kumzingira kwa kumpiga na kusababisha watu hao sita kujeruhiwa.

Taarifa iliyotolewa juzi na Kamanda wa Polisi mkoani Shinyanga, Deborah Magiligimba, ilisema baada ya watu hao kujeruhiwa walikimbizwa hospitali kupatiwa matibabu na hali zao zinaendelea vizuri.

Aliwataja waliojeruhiwa kuwa ni Zengo Jitonja, Nkuba Deteba, Juma Salaganda, Limbu Mihambo, Dutu Mdese, na John Matanda.

"Watu hawa wakati wakiwa wamemzingira fisi huyo na kuanza kumshambulia, aliwang'ata sehemu mbalimbali za miili yao, majeruhi watano walipata majeraha madogo na wemeruhusiwa kutoka hospitali," alisema Magiligimba.

"Majeruhi mmoja Nzengo Jintonja, ambaye alijeruhiwa vibaya kwa kung'atwa mikononi na mdomoni, yeye alikimbizwa na kulazwa katika Hospitali ya Rufani ya Mkoa wa Shinyanga na hali yake siyo mbaya sana," aliongeza.

Alisema fisi huyo ameshauawa na wananchi walioendelea kumshambulia kwa kumpiga.

Habari Kubwa