SMZ yafunguka kuvuja mitihani

06Dec 2018
Rahma Suleiman
Zanzibar
Nipashe
SMZ yafunguka kuvuja mitihani

WIZARA ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, imeibuka na kusema kitendo cha kuvuja kwa mitihani ya kidato cha pili ni dalili kwamba maadili ya kazi na uaminifu  wa kutunza siri vimeporomoka.

Naibu Waziri wa wizara ya elimu smz, Mmanga Mjengo Mjawiri, (aliyesimama) picha na mtandao

Naibu Waziri wa wizara hiyo, Mmanga Mjengo Mjawiri, alisema hayo jana alipokuwa akitoa ufafanuzi kuhusu suala la kufutwa kwa mitihani ya kidato cha pili baada ya kubainika kuwa imevuja.  

Alisema usimamizi wa mitihani na matayarisho yake kwa ujumla, vinaongozwa na maadili ya kazi ikiwamo kutunza siri kwa watendaji wanaotunga mitihani hiyo.  

“Wizara ya Elimu imesikitishwa na tukio hilo ambalo linaonyesha wazi kwamba maadili ya kazi na uaminifu wake katika kutunza siri za serikali yamepungua kwa kiwango kikubwa,” alisema.  

Hatua ya kuvuja kwa mitihani hiyo imesababisha na sasa wizara iko katika maandalizi ya matayarisho ya mitihani mingine, huku uchunguzi dhidi ya watendaji waliohusika na kadhfa hiyo ukifanywa na vyombo vya sheria.  

Naye Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Mohamed Aboud Mohamed, aliwaambia wajumbe wa Baraza la Wawakilishi kwamba serikali itachukuwa hatua kali kwa watendaji waliohusika na uvujishaji wa mitihani hiyo.

  Alisema kitendo kilichofanywa na watumishi hao kimeitia hasara kubwa serikali kwa kulazimika kutayarisha mitihani mingine, lakini kimesababisha usumbufu mkubwa kwa wanafunzi na wazazi kwa ujumla.  

“Mheshimiwa Spika napenda kuliarifu Baraza la Wawakilishi kwamba serikali inalifahamu tukio la kuvuja kwa mitihani ya kidato cha pili na kufutwa. Kwa sasa uchunguzi mkali unaendelea ili kujua watu waliohusika na tukio hilo, ili wachukuliwe hatua za kisheria,” alisema.

Mitihani ya kidato cha pili Zanzibar iliyoanza kufanyika Jumatatu wiki hii, ilifutwa baada ya kubainika kuwapo udanganyifu ikiwamo kuvuja kwake katika baadhi ya maeneo.

Kutokana na hali hiyo, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali, Riziki Pembe Juma, alitangaza kufutwa kwa mitihani hiyo kwa kile alichosema ni kutenda haki na usawa kwa wote.

Waziri huyo alisema kutokana na kuvuja huko, serikali imepata hasara ya Sh. milioni 250, ambazo zilitumika kwa ajili ya uchapishaji.

Habari Kubwa