Soma ujiajiri inapasua kichwa!

24Jan 2021
Joseph Kulangwa
Dar es Salaam
Nipashe Jumapili
Soma ujiajiri inapasua kichwa!

HAKUNA kitu kinachosumbua vichwa vya watu kama mtihani. Mtihani wa kitu chochote ambacho mwishowe ni matokeo ya jinsi mtahini walivyofanya.

Wasiwasi huwajaa sana watahiniwa wanapokaribia siku za mitihani, si shuleni wala vyuoni, si sehemu za kazi. Mtihani ni pamoja na usaili wowote uwe wa ajira au wa polisi.

Lakini matokeo mazuri ya mitihani, huzalisha furaha isiyo na kifani kwa mhusika. Ndiyo sababu hata zawadi hutolewa kwa aliyefanya vizuri kwenye mtihani wowote, na mfaulu hujisikia vema sana.

Hakuna mzazi anayesikitika anapoambiwa mwanao kafaulu mtihani hata uwe wa darasa la saba. Mzazi hufunguka na hata kama hana kitu, hujikamua ili kuonyesha furaha yake na kumzawadia mtoto.

Furaha haishii ngazi ya familia, bali hufika hata ngazi ya kitaifa, ambapo wahusika wanaosimamia elimu hujisikia faraja zaidi wanapoona wanafunzi wamefaulu mitihani yao, na ndiyo sababu kila mwaka watatoa alama za ufaulu kwa asilimia.

Hujisikia vema sana waonapo ufaulu wa mwaka huu umepita wa mwaka uliotangulia, na kujipa matumaini kwamba kiwango cha elimu kimepanda ama kutokana na walimu kufundisha vizuri au wanafunzi kujibidiisha, au yote.

Zamani mtoto alipofaulu, mzazi alijipa matumaini ya ukombozi kwamba tayari anaandaa mtu ambaye atamaliza masomo yake na hatimaye apate ajira, amsaidie pamoja na familia nzima.

Enzi hizo hata aliyemaliza darasa la saba alipata ajira, kama si ualimu hata kazi ya jeshi ilimhusu. Hivyo ilikuwa faraja sana kuona mtoto akimaliza shule na kupata ajira na kujitegemea.

Vivyo hivyo kwa aliyemaliza darasa la 12 na aliyehitimu la 14; leo utasikia fomfoo au fomsiksi. Ilikuwa neema sana kwa mtoto kuvuka kote huko na kufikia chuo cha kati au kikuu, kwani uhakika wa kazi yenye maslahi makubwa ilikuwa dhahiri.

Ni wakati huo ambapo wahitimu wa darasa la saba mpaka vyuo vikuu, hawakuwa wakionekana mitaani wakisaka ajira! Haikuwa hivyo, kwani aliyemaliza darasa la 12 alitakiwa kujaza fomu maalumu za ajira, kwa kuwa ilikuwa lazima aajiriwe. Vivyo hivyo kwa darasa la 14.

Enzi hizo wahitimu hao walikuwa wachache, kwa kuwa shule zenyewe hususan za sekondari nazo zilikuwa chache. Kwa hiyo waajiriwa walikuwa wachache huku nafasi zikiwa nyingi, hususan serikalini.

Ndio wakati ambao serikali ilikuwa ina kila kitu, kuanzia shule, vyuo, ofisi za kiutawala, viwanda na mashirika. Hivyo wahitimu wote walimezwa humo. Kwa kifupi ajira zilikuwa za uhakika, ili mradi umalize shule au chuo kwa ufaulu uliotakiwa.

Polepole mambo yalianza kubadilika. Wanafunzi wakawa wengi katika shule za msingi, wahitimu wa darasa la saba wakaongezeka, wakati ambao ajira zikawa zinawatazama wa sekondari zaidi na vyuo.

Kana kwamba haitoshi, polepole hivyo hivyo, wahitimu wa sekondari nao wakaongezeka. wale wa fom foo nao wakajaa mitaani, ajira zikaenda kwa fom siksi. Kidogo kidogo wa fom siksi nao wakatupwa na wakati, ukimaliza hakuna kujaza fomu za ajira (Sel Forms), ajira zikawa za vyuo vya kati na kasha vyuo vikuu.

Hivi sasa inaonekana dhahiri wa vyuo nao wametupwa na wakati. Hivi sasa maliza rudikwa baba na mama yako, hangaika mwenyewe. Huku ukisikilizia mirindimo ya nyimbo za “jiajirini…msisome mkitarajia kuajiriwa na serikali…kuweni wajasiriamali…”

Nyimbo hizo hivi sasa zimezoeleka, huku mafunzo yatolewayo vyuoni hayawaandai wengi kujiajiri, kwa sababu mfumo wao bado ni wa kuajiriwa serikalini. Walimu, madaktari, wahandisi, watawala, na kadhalika. Ndiyo bado wanafundishwa vyuoni na kutakiwa kurudi nyumbani kujiajiri!

Itafika wazazi wataanza kuona elimu ni kupoteza muda na fedha, bora mabinti waolewe kama ilivyokuwa zamani au mabinti wabaki nyumbani kuchunga mifugo, kwa kuwa hata wakienda huko kunakoitwa vyuo, hatimaye watarudi nyumbani kutafuta cha kufanya.

Wenye dhamana waangalieni nini cha kufanya kuhusu elimu yetu, ili iwaandae watoto kuwa na cha kufanya kinachoendana na miaka wanayotumia wakiwa vyuoni. Tunashindwa nini wakati tuko katika uchumi wa kati bhana? Alamsiki!

Habari Kubwa