Somo murua kwa madhehebu ya dini

08Oct 2017
Robert Temaliwa
Nipashe Jumapili
Somo murua kwa madhehebu ya dini

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa, ameyataka madhehebu ya dini nchini kuhubiri amani ili kuendeleza ustawi uliopo nchini pamoja na amani na uvulivu.

Sambamba na hiyo, ameipongeza Jumuiya ya Waislamu wa Ahmadiyya kutokana na juhudi kubwa inazozifanya katika kuhubiri upendo na amani muda wote kwa wanaumini wao bila kuchoka.

Akizungumza juzi kwenye mkutano wa 48 wa jumuiya hiyo uliofanyikia eneo la Kitonga, Ilala jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na zaidi ya waumini 3,000 kutoka mikoa mbalimbali ya Tanzania na nchi jirani, Majaliwa alisema  madhehebu mengine yanatakiwa kuiga mfano huo ili kuendelea kudumisha amani iliyopo nchini.

Majaliwa alisema serikali haina budi kuipongeza jumuiya hiyo kutokana na inavyoubiri upendo na amani muda wote, hivyo kuunga juhudi za serikali katika kuhamasisha amani nchini.

Alisema mbali ya jumuya hiyo kuwa mfano wa kuigwa katika kuhubiri upendo na amani lakini pia imekuwa mstari wa mbele katika kuchangia maendeleo nchini.

"Kwa kweli sina budi kuipongeza jumuiya hii kwa jinsi mnavyohubiri upendo na amani muda wote na pia mnavyoisaidia serikali katika kuchangia masuala mbalimbali ya maendeleo nchini, " alisema Majaliwa.

Alisema madhehebu yote yaendelee kusaidia kuhubiri upendo na amani bila ya kubaguana ili kulinda lulu ya amani iliyopo nchini huku wakiwapiga vita wasiopenda amani.

Majaliwa alisema serikali haifungamani na dini yoyote  zaidi ya kuheshimu dini zote ndiyo maana imetoa uhuru wa kila mwananchi kuabudu dini anayoitaka. 

Aliwataka viongozi wa dini mbalimbali kutojihusisha na masuala ya kisiasa kwa kuwaepuka wanasiasa wanaotaka kuwaingiza kwenye uvunjifu wa amani.

Habari Kubwa