Sophia Simba apeta ubunge CCM

12Aug 2020
Augusta Njoji
Dodoma
Nipashe
Sophia Simba apeta ubunge CCM

MWENYEKITI wa Jumuiya ya Wanawake ya CCM (UWT) na Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM aliyefukuzwa uanachama na baadaye kurejea tena, Sophia Simba, ameonyesha kurejea tena katika duru za siasa nchini baada ya kupenya kwenye tatu bora za kuwania ubunge wa viti maalum.

Juzi, Sophia katika kura za maoni za kuwasaka wabunge wa viti maalum kuwakilisha taasisi zisizo za kiserikali (NGOs), alishika nafasi ya tatu baada ya kupata kura 43.

Kundi hilo lilikuwa na wagombea 21 na nafasi zilizokuwa zikiwaniwa ni tatu, Neema Lugangila akiongoza kwa kura 60 akifuatwa na aliyewahi kuwa Waziri wa Viwanda na Biashara, Rita Mlaki, aliyepata kura 48.

Kundi la vyuo vikuu, wagombea 21 walipigiwa kura za maoni kuwania nafasi tatu. Msimamizi Mkuu wa Uchaguzi huo, Salum Khatib Reja, alimtangaza Paulina Nahato kuongoza kwa kura 75, akifuatwa na Aziza Msuya (70) na Thea Ntara (44).

Katika kundi la watu wenye ulemavu, Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Watu Wenye Ulemavu), Stella Ikupa, aliongoza kwa kupata kura 94 akifuatwa na Khadija Taya (39) na Ummy Ndeliyananga (38).

Wagombea 23 walijitosa kuwania ubunge wa viti maalum kupitia kundi la vyama vya wafanyakazi, Alice Kaijage akioongoza kwa kura 77, akifuatwa na Jenejeri Ntate (32) na Lucy Mwakyembe (28).

Kwa upande wa viti maalum kupitia kundi la vyuo vikuu katika Baraza la Wawakilishi Zanzibar, walioongoza kura za maoni ni Mariam Khamis (103), Saada Ramadhan (86) na Riziki Juma (59).

Vilevile, katika kuwania ubunge wa viti maalum kupitia kundi la watu wenye ulemavu katika baraza hilo, walioongoza kura za maoni ni Mwantatu Khamis aliyepigiwa kura 122, akifuatwa na Zainab Salum (55) na Fatma Shaibu (46).

Habari Kubwa