Spika aibana serikali  utaifishaji ng'ombe

23May 2018
Sanula Athanas
DODOMA
Nipashe
Spika aibana serikali  utaifishaji ng'ombe

SPIKA wa Bunge, Job Ndugai ameitaka serikali kuutazama upya utaratibu wa kutaifisha na kupiga mnada mifugo inayokamatwa kwenye maeneo ya hifadhi kwa kuwa umekuwa ukisababisha umaskini kwa wafugaji.

SPIKA wa Bunge, Job Ndugai.

Kiongozi huyo wa Bunge alisema hayo bungeni jijini Dodoma jana muda mfupi kabla ya kuahirisha kikao cha mchana.

Alisema utaratibu huo pia umekuwa ukisababisha ukatili dhidi ya ndama wanaoachwa nyumbani baada ya 'wazazi wao' kukamatwa kwenye hifadhi na kupigwa mnada.

"Ile mifugo wakati mwingine imetoka kwa babu, baba, na yeye na familia. Kwa sababu tu wamekanyanga hifadhi, wote wanauzwa," Spika Ndugai alisema.

"Ni ngumu hata kuamini, yule mzee anarudi nyumbani na fimbo yake tu, anarudi nyumbani anakuta vile vindama vinalia, mama zao wameuzwa kwenye hifadhi. 

"Vindama vingine vina wiki mbili tangu vizaliwe, ni lazima vitakufa tu, utavifanyaje vile? Hatuwezi kufanya hivyo Tanzania jamani. Hata kama mkichukua nusu, si ni adhabu tosha. 

"Yaani mnachukua wote kweli. Ni kama wewe una nyumba zako na magari yako, yote yanachukuliwa unabaki huna kitu, utajinyonga au utabaki? Hili kwa kweli hapana!" 

Katika majibu yake kuhusu hoja hiyo jana jioni, Waziri wa Katiba na Sheria, Prof. Paramagamba Kabudi, alisema sheria inatamka wazi kuwa mifugo ikishaingia kwenye hifadhi za serikali itaifishwe.

Hata hivyo, alisema serikali imeona changamoto zilizojitokeza kutokana na kutekelezwa kwa sheria hiyo na imeamua kuiachia baadhi ya mifugo na kuirejesha kwa wafugaji.

Prof. Kabudi pia alibainisha kuwa atakutana na Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Jaji Mkuu ili kuangalia namna ya kutatua changamoto ya utunzaji wa ushahidi wa kesi zinazofunguliwa kuhusu ng'ombe wanaokamatwa kwenye hifadhi.

Alisema kumekuwa na changamoto ya urejeshaji wa mali za wafugaji pale wanaposhinda kesi maana ng'ombe wao wanakuwa wameshauzwa na wengine kufa wakati kesi zikiwa hazijatolewa hukumu.

Habari Kubwa