Spika ataka taarifa maafa ya mafuriko

01Apr 2020
Augusta Njoji
Dar es Salaam
Nipashe
Spika ataka taarifa maafa ya mafuriko

SPIKA wa Bunge, Job Ndugai, ametaka serikali kujipanga kutoa taarifa rasmi bungeni kuhusu maafa yaliyotokea nchini kutokana na mvua kubwa inayoendelea kunyesha.

SPIKA wa Bunge, Job Ndugai, picha mtandao

Kiongozi huyo wa Bunge alitoa agizo hilo jana, bungeni jijini hapa, alipojibu hoja ya Mbunge wa Rufiji (CCM), Mohamed Mchengerwa, aliyeitaka serikali kulitaarifu Bunge hatua inazochukua kuwasaidia wananchi wa Rufiji ambao sasa hawana makazi kutokana na mvua hiyo.

Mchengerwa alisema kutokana na mvua hiyo, hadi sasa wananchi wanaokadiriwa kuwa kati ya 20,000 na 50,000 hawana makazi, chakula na wanahangaika kuokoa maisha yao.

“Je, kama Bunge tunachukua hatua gani ili kuwaangalia hata hawa wananchi wanyonge ambao wako kwenye maafa ya mafuriko?" Mchengerwa alihoji.

Akijibu hoja hiyo, Spika Ndugai alitoa pole kwa wananchi wa Rufiji na Kibiti kutokana na baa hilo na kusema kuwa mafuriko ya aina hiyo yaliyotokea katika eneo hilo ni ya aina yake kulinganishwa na miaka ya nyuma.

“Ni maafa makubwa sana, ninaamini serikali imesikia ujumbe wa mbunge na serikali imekuwa ikiendelea kuchukua hatua mbalimbali na wakati fulani utafika tutaiomba serikali kutoa taarifa juu ya mipango inayoendelea nayo.

“Tunapokea ushauri wake Mheshimiwa Mbunge, na Mheshimiwa Jenista (Mhagama) ambaye ndiye Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya maafa, yako chini yake, wakati utakapofika, atatupa taarifa kama Bunge kuhusu maafa haya,” aliagiza.

Habari Kubwa