Spika Ndugai kushtakiwa kortini kisa CAG

13Jan 2019
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe Jumapili
Spika Ndugai kushtakiwa kortini kisa CAG

Zitto Kabwe na wabunge wengine wanne wanatarajia kufungua kesi ya kikatiba Mahakama Kuu ili kupata tafsiri ya kisheria, juu ya mipaka ya kinga ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) na mamlaka ya Spika kumshtaki mwananchi bila kuathiri uhuru wa maoni ya kikatiba.

zitto kabwe mbunge wa kigoma mjini act-wazalendo, picha mtandao

Zitto Kabwe na wabunge wengine wanne wanatarajia kufungua kesi ya kikatiba Mahakama Kuu ili kupata tafsiri ya kisheria, juu ya mipaka ya kinga ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) na mamlaka ya Spika kumshtaki mwananchi bila kuathiri uhuru wa maoni ya kikatiba.

Mbunge huyo wa Kigoma Mjini (ACT-Wazalendo) amefichua mpango huo alipozungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo.

Amesema wanaona ni muhimu CAG kutotii amri ya Spika Job Ndugai ya kumtaka kufika mbele ya Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge kuhojiwa kutokana na kauli yake kwamba anafikiri "Bunge ni dhaifu".

Zitto amewataja watakaoungana naye kufungua kesi hiyo kuwa ni Mbunge wa Ubungo, Saed Kubenea (Chadema), Mbunge wa Viti Maalum Shinyanga Mjini, Salome Makamba (Chadema), Mbunge wa Mchinga, Hamidu Bobali (CUF), na Mbunge wa Moshi Vijijini, Anthony Komu (Chadema).

Amesema wameamua kufungua kesi hiyo ili kuiomba mahakama itoe tafsiri ya kinga ya CAG iliyopo kikatiba na pia kutoa tafsiri ya Sheria ya Haki, Kinga na Madaraka ya Bunge katika kushtaki watu wanaosemekana kudharau Bunge.

Kiongozi huyo wa ACT-Wazalendo pia amesema watahoji mahakamani mamlaka ya Spika wa Bunge kumwita mtu yeyote kuhojiwa kwenye Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge pasi na azimio la Bunge zima.

Zitto amesema wameamua kufungua kesi ili kuiomba Mahakama Kuu imzuie CAG kutii amri ya Spika na kumkataza Spika kutekeleza wito wake kwa CAG kwa kuwa ni kinyume cha katiba.

Habari Kubwa