Spika Tulia akunwa uwekezaji CRDB

21May 2022
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Spika Tulia akunwa uwekezaji CRDB

SPIKA wa Bunge la Tanzania, Dk. Tulia Ackson, ameipongeza Benki ya CRDB kwa kuendelea kutengeneza faida kubwa inayoiwezesha kutoa gawio kwa wanahisa wake kutokana na uwekezaji inaoufanya.

Dk. Tulia alitoa pongezi hizo wakati akifungua semina ya elimu ya fedha iliyoandaliwa na benki hiyo kwa wanahisa na Watanzania kuelekea Mkutano Mkuu wa 27 wa Wanahisa utakaofanyika Mei 22, katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Arusha (AICC).

“Nadhani sitakuwa nimekosea nikisema ongezeko la faida baada ya kodi ambayo Benki yetu ya CRDB imepata mwaka jana kufikia Sh. bilioni 236 kulinganisha na Sh. bilioni 165 mwaka 2020, ni ukuaji mkubwa wa faida kupata kutokea,” alisema Dk. Tulia.

Alisema CRDB imeendelea kudhihirisha Kwa vitendo kuwa “benki kiongozi” nchini kwa kuwa kila mwaka imekuwa ikiendelea kutoa faida ya uwekezaji kwa wanahisa wake huku akizitaka taasisi nyengine za umma na binafsi kuiga mfano.

“Nimefurahishwa pia kusikia mwaka huu Bodi ya Wakurugenzi imekuja na pendekezo la ongezeko la asilimia 64 ya gawio kwa hisa. Wanahisa wa CRDB mnastahili kutembea kifua mbele kwa ongezeko hili,” aliongeza.

Dk. Tulia pia aliipongeza CRDB kwa kuandaa semina ya elimu ya fedha na uwekezaji kwa ajili ya wanahisa wake na Watanzania huku akibainisha kuwa umahiri wa masuala ya fedha wa wananchi ni moja ya misingi muhimu ya maendeleo ya watu wa taifa lolote duniani.

“Niwapongeze CRDB kwa kuongoza katika utoaji wa elimu ya masuala ya fedha kwa Watanzania. Siku chache zilizopita, mliandaa semina mliyoiita CRDB Bank Uwekezaji Day. Mimi  niliichungulia mtandaoni nikiwa Dodoma,” alisema  Dk. Tulia huku akiitaka benki hiyo kuendelea kutoa elimu kwa wananchi ili kuongeza ujumuishi wa kifedha.

Pia aliitaka CRDB kuendelea kuwekeza katika kuendelea kuwezesha sekta mbambali za maendeleo nchini hususan sekta ya kilimo, huku akiitaka pia kusaidia malengo ya serikali katika uanzishwaji wa Benki ya Ushirika ya Taifa kama ambavyo imefanya kwa Benki ya Ushirika ya Tandahimba (TACOBA) na Benki ya Ushirika ya Kilimanjaro (KCBL).

Dk. Tulia pia aliitaka benki kuendelea na jitihada za uwezeshaji wa kundi la vijana ili kuchochea ukuaji wa ajira nchini.

Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya CRDB, Dk. Ally Laay, alisema benki hiyo ikiwa ya kizalendo inayomilikiwa na Watanzania kwa zaidi ya asilimia 80, inajivunia kuendelea kukuza thamani ya uwekezaji wa wanahisa wake ikiwamo Serikali ambayo inamiliki asilimia 36 ya hisa katika benki hiyo.

“Niwakaribishe Watanzania wengine waje kuwekeza ndani ya benki yetu ili nawao waanze kunufaika na gawio nono ambalo limekuwa likitolewa na benki yao,” alisema  Dk. Laay.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB, Abdulmajid Nsekela, alisema malengo ya semina hiyo ni kuwajengea uwezo wanahisa na Watanzania wengine ili kuwajengea uwajibikaji wa kifedha na kuongeza ushiriki katika fursa za uwekezaji hususan katika Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE).

“Kwa kutoa elimu hii wanahisa wetu pia wanapata kufahamu zaidi faida za kuwekeza katika Benki yao ya CRDB, hivyo basi kuongeza uwekezaji na kupata faida nono zaidi, lakini pia kuwahamasisha na Watanzania wengine pia kuwekeza katika hisa hususan za Benki ya CRDB na kuanza kupata gawio,” alisema.

Nsekela alitumia fursa hiyo pia kuwakaribisha Wanahisa katika Mkutano Mkuu utakaofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano (AICC) na kupitia Mtandao. “Mkutano utaanza saa 3 asubuhi, watu wa mtandaoni wataweza kujiunga kupitia link https://escrowagm.com/crdb/login.aspx au kupitia SimBanking App,” alisema Nsekela.

Habari Kubwa