Staili za wagombea kuomba kura zawa kivutio

28Sep 2020
Thobias Mwanakatwe
Dar es Salaam
Nipashe
Staili za wagombea kuomba kura zawa kivutio

KAMPENI za uchaguzi mkuu unaotarajia kufanyika Oktoba 28, mwaka huu, zimeonekana kuweka rekodi mpya ukilinganisha na uchaguzi uliopita kutokana na 'staili' zinazotumiwa na wagombea katika kuomba kura kwa wananchi katika maeneo mbalimbali.

Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili katika maeneo mbalimbali ya kampeni umebaini kuwa baadhi ya wagombea kutoegemea mikutano ya hadhara ya kampeni pekee na badala yake wanatumia staili za kusaka kura kwa kuwafikia wananchi kwenye makundi tofauti.

Baadhi ya staili zinazotumiwa na wagombea kuomba kura ni kutembelea vibanda vya mamalishe, saluni za kike, sokoni, kutumia usafiri wa punda na pikipiki.

Miongoni mwa wagombea ambaye amekuwa na ubunifu wa kipekee wa kusaka kura na kuwa kivutio kwa wananchi ni mgombea ubunge Jimbo la Ukonga kwa tiketi ya CCM, Jerry Slaa.

Slaa ameonekana kuomba kura kwa wananchi kwenye saluni za kike na kivutio zaidi ni kushiriki kuwahudumia wateja kwenye saluni hizo.

Katika moja ya picha iliyosambazwa kwenye mitandao ya kijamii ameonekana akimhudumia msichana kwa kumtengeneza kucha za miguu kwenye saluni moja huko Jimbo la Ukonga.

Mgombea huyo katika picha nyingine ameonekana akisaka kura kwa kushiriki kupakua chakula kwa wateja kwenye vibanda cha mamalishe na kushona viatu kwa mafundi.

Maoni ya wananchi yanaonyesha kuwa mgombea huyo ndiye anaongoza kwa kuwa staili za kipekee katika kuomba kura kwa wapigakura wa Jimbo la Ukonga.

Mgombea ubunge Jimbo la Temeke kupitia CCM, Dorothy Kilave, naye alionekana kuendesha kampeni kwa staili ya kusuka wateja kwenye saluni za kike.

Mgombea ubunge wa Tarime Vijijini kwa tiketi ya CCM, Mwita Waitara, amekuwa akitumia pikipiki kwa kuendesha mwenyewe kusaka kura kwa wananchi.

Waitara ambaye ni Naibu Waziri Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, amekuwa kivutio kwa wananchi wa jimbo hilo kwa kuomba kura kwa kuendesha pikipiki.

Kadhalika, staili ya viongozi wa CCM kuomba kura kwa staili ya kuwapigia magoti wananchi, mbunge anayemaliza muda wake wa Viti Maalum Mkoa wa Mbeya, Mary Mwanjelwa, ndiye anayeongoza.

Katika kila jimbo mkoani Mbeya, Mwanjelwa, amekuwa akiwaombea kura wagombea kwa kupiga magoti kuonyesha unyenyekevu kwa wananchi.

Mgombea udiwani Kata ya Segerea kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Marysponsa Mbilinyi naye amekuwa kivutio kwa staili yake ya kuomba kura kwa mam lishe, waendesha pikipiki (bodaboda) na saluni.

Habari Kubwa