Stika kuwekwa bidhaa kutoka nje

17May 2018
Mary Geofrey
DAR ES SALAAM
Nipashe
Stika kuwekwa bidhaa kutoka nje

Shirika la Viwango Tanzania (TBS) lipo mbioni kuanza kuweka alama maalumu ya stika kwenye bidhaa zote zilizokaguliwa kutoka nje ya nchi na zilizothibitishwa ubora wa viwango na shirika hilo ili kulinda watumiaji.

Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano wa TBS, Rhoida Andusamile.

Hayo yalisemwa Dar es Salaam na Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano wa TBS, Rhoida Andusamile, akizungumza na waandishi wa habari wakati wa kuteketeza betri za umeme wa solar ambazo zimethibitishwa na shirika hilo kutokidhi viwango vya ubora.

Alisema pamoja na mikakati mingine inayochukuliwa na shirika hilo kuondoa bidhaa ambazo hazina ubora kwenye soko, kwa sasa shirika hilo lipo kwenye mchakato wa mwisho wa kuanza kuweka stika kwenye bidhaa zinazotoka nje, ambazo zimethibitishwa ubora ili kuwasaidia Watanzania.

“Tutaanza kufanya kama tunavyofanya kwenye bidhaa zinazozalishwa hapa kwetu, ambapo zinakuwa na alama yetu ya ubora, hivyo na bidhaa kutoka nje ambazo zimethibitishwa ubora zitakuwa na stika  maalumu,” alisisitiza Andusamile.

Akizungumzia betri za umeme jua zilizoteketezwa, alisema zilikuwa jumla ya betri 157 zenye thamani ya Sh. milioni nane na zilipatikana kwenye maduka mawili yaliyopo Kariakoo, jijini Dar es Salaam.

“Betri hizi tumeziondoa kwenye soko  kwa gharama za wenye mzigo na tunazoteketeza ni kwa gharama zao wenyewe,” alisema.   

Habari Kubwa