SUA kutengeneza chanjo ya corona

05Aug 2021
Ashton Balaigwa
Morogoro
Nipashe
SUA kutengeneza chanjo ya corona

CHUO Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) na Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili kwa kushirikiana Taasisi ya Taifa ya Utafiti ya Magonjwa ya Binadamu (NIMR) wameanza kufanya utafiti wa chanjo ya virusi vya corona, ili wazalishe chanjo hiyo nchini.

Akizungumza katika uzinduzi wa utoaji wa chanjo dhidi ya ugonjwa wa UVIKO-19 katika chuo hicho jana, Makamu Mkuu wa SUA, Prof. Raphael Chibunda, alisema lengo la kuzalisha chanjo hiyo ni kukidhi mahitaji ya chanjo nchini, ili isiagizwe kutoka nje ya nchi.

Alisema kwa sasa chanjo zote zilizoanza kutumika nchini zimeletwa kutoka nje ya nchi, lakini wao kama wasomi nchini kwa kutumia nafasi yao ya sehemu ya vyuo vikuu, wameona kuna haja kuanza kufanya utafiti wa pamoja, ili kukidhi mahitaji ya chanjo za ugonjwa huo, ambazo zitazalishwa nchini.

“Sisi kama sehemu ya taasisi za elimu ya juu nchini, tumeona tushirikiane na vyuo vingine vikuu kama Muhimbili na Taasisi ya NIMR tuanze sasa kuzalisha chanjo ya virusi vya corona, ili kuisaidia kupunguza makali na madhara ya virusi hivyo kwa taifa," alisema.

Akizungumzia kuhusu utoaji wa chanjo hiyo kwa jamii nzima, alisema baada ya chanjo hizo kupatikana katika Mkoa wa Morogoro, waliwasilisha ombi la kuwa na kituo katika chuo hicho kutokana na idadi kubwa ya wanafunzi wapatao 15,000, pamoja na wafanyakazi 2,000, ambao wengi wao umri wao ni mkubwa.

Alimshukuru Mkuu wa Mkoa wa Morogoro pamoja na Ofisi ya Mganga Mkuu wa Mkoa kwa kukubali kuanzisha kituo hicho na kuwapa chanjo 500, kwa ajili ya hatua za mwanzo za kuchanja makundi maalum yenye sifa.

Profesa Chibunda alisema pamoja na uhaba wa chanjo walizopata, wanaamini wataongezewa kadri siku zinavyoendelea na watakavyopokea na kuitaka jamii kupuuza na kuacha kupotoshwa na baadhi ya watu katika mitandao kuwa chanjo hiyo ina madhara.

“Maprofesa hao wanachanjwa hapa ndio wamekuwa wakisafiri katika nchi nyingi duniani, sasa kama hii chanjo ingekuwa na madhara yoyote, wao ndio wangekuwa wa kwanza kutochanja, hebu tuachane na watu wanaopotosha kuhusu chanjo hii," alisema.

Bingwa wa Magonjwa ya Moyo na Kiongozi wa Madaktari wa Hospitali ya SUA, Dk. Omary Kasuwi, alisema anashukuru kupatikana kwa chanjo hiyo ya UVIKO-19, kwa kuwa itasaidia kupunguza kero za wagonjwa waliokuwa wakifika kupata matibabu katika hospitali hiyo.

Dk. Kasuwi alisema hospitali hiyo inayohudumia wanafunzi wa SUA, wafanyakazi na watu kutoka nje imeshapokea takribani wagonjwa 2,000, tangu kuibuka kwa ugonjwa huo wa corona na kuwapatia matibabu mbalimbali.