Sugu ampongeza Mwakyembe, atoa tahadhari uchaguzi wa 2020

17Jun 2019
Sanula Athanas
DODOMA
Nipashe
Sugu ampongeza Mwakyembe, atoa tahadhari uchaguzi wa 2020

MBUNGE wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi 'Sugu' (Chadema), amempongeza Waziri wa Habari, Utamaduni Sanaa na Michezo, Dk. Harrison Mwakyembe, kutokana na mafanikio makubwa yaliyopatikana katika sekta ya sanaa na burudani mwaka huu.

MBUNGE wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi 'Sugu'.

Akiwasilisha bungeni jijini Dodoma hivi karibuni, makadirio ya mapato na matumizi ya wizara yake kwa mwaka ujao wa fedha, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango, alisema sekta hiyo imeongoza sekta zote kwa kasi ya ukuaji kiuchumi mwaka huu.

Dk. Mpango alisema sekta hiyo mwaka huu imekua kwa asilimia 13.7 ikifuatwa na sekta za ujenzi asilimia 12.9, uchukuzi na uhifadhi wa mizigo asilimia 11.8 na habari na mawasiliano asilimia 9.1.


Katika mahojiano maalum na Nipashe bungeni jijini Dodoma wiki iliyopita, Sugu alisema kuwa pamoja na kwamba yeye ni mbunge wa upinzani, anampongeza Dk. Mwakyembe kwa mafanikio hayo, akieleza kuwa yametokana na waziri huyo kufanyia kazi ushauri wa wabunge.

Mbali na kumpongeza mtaalamu huyo wa sheria, Sugu pia alizungumzia hukumu ya kutumikia kifungo cha miezi sita gerezani aliyopewa hivi karibuni kisha kuachiwa kwa msamaha wa Rais John Magufuli. Katika mahojiano hayo, Sugu ambaye pia ni Waziri Kivuli wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, alizungumzia hali ya kisiasa nchini, hususan upinzani mkali wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) unaomkabili katika kuwania tena ubunge wa Jimbo la Mbeya Mjini.Ifuatayo ni sehemu ya mahojiano ya Nipashe na mbunge huyo:SWALI: Sekta ya sanaa na burudani imeongoza kwa kasi ya ukuaji kiuchumi mwaka huu. Wewe ni msanii na ni waziri kivuli katika wizara inayosimamia sekta hii, mafanikio hayo yamechochewa na kipi hasa?


SUGU: Kwa kweli ni mafanikio 'positive' (chanya) na kitu ambacho tumekuwa tukikipigania miaka mingi. Ni kwamba juhudi zilikuwapo na hayo yanayoitwa mapato yalikuwapo. Shida yetu si kwamba mapato hayakuwapo, shida yetu ilikuwa kwamba hayakuwa na udhibiti na ufuatiliaji.

Kwa hiyo, mapato yalikuwa hayawafikii walengwa ambao ni wasanii, lakini pia serikali ilikuwa haifikiwi na mapato haya kwa maana ya kodi.

Na ndiyo maana tukawa tunasisitiza sanaa irasmishwe kwa sababu ikishakuwa rasmi, inakuwa rahisi kwa serikali kuifuatilia, na ukishaifuatilia, utaisimamia vizuri na ukiisimamia utapata kilicho cha kwako na walengwa watapata kilicho cha kwao.

Kwa hiyo, mafanikio hayo si kwamba yametokea kwa bahati mbaya, yametokana na kazi ambayo tumekuwa tukiifanya humu bungeni.

Nipeleke tu 'credits' (pongezi) kwa Mheshimiwa Waziri (Dk. Mwakyembe) kwa sasa kwa kuwa pamoja na kutokusema, lakini amekuwa akichukua ushauri wetu.


SWALI: Unafikiri mafanikio haya ni ya msanii mmoja mmoja?SUGU: Hapana! Ni 'collective' (kwa ujumla). Hata unaposema kilimo kimefanikiwa, haimaanishi kwamba wakulima wote wako sawasawa.Sasa tunajua kama wasanii eneo letu lina mapato kiasi gani. Ni kazi yetu sisi kama wasanii mmoja mmoja kupigana kupata kipande katika zile 'revenues' (mapato) zote.SWALI: Kwa hali ilivyo kisiasa nchini, matumaini ni makubwa kiasi gani kwamba utarejea bungeni baada ya uchaguzi mkuu wa mwakani?SUGU: ... (kicheko) Nikuhakikishie tu kwamba Sugu atakuwapo bungeni baada ya Uchaguzi Mkuu wa 2020. Hapa katikati yetu na mwaka 2020 wa uchaguzi, kuna Mungu tu, hakuna binadamu atakayezuia. Na hilo tumeshalisema wazi - suala la ubunge wa Jimbo la Mbeya Mjini si Sugu kuwa mbunge. Suala lililopo Mbeya ni kura za Mbeya zinachangia vipi katika kura za kitaifa ii kuing'oa serikali ya CCM. Hiyo ndiyo hoja ya wanaMbeya, kwamba kura zao zinatoa mchango gani katika kuing'oa CCM madarakani 2020 na si suala la mbunge. Suala la Mbunge wa Mbeya Mjini tulishalimaliza tangu mwaka 2010. Kilichotokea mwaka 2015, ndicho kitakachotokea mwaka 2020 na ndiyo maana nasema, kati yetu na uchaguzi wa mwaka 2020, hatuna binadamu wala mtu yeyote mbali kuna Mungu tu! Ni suala la kuomba uzima.
SWALI: Kifungo cha miezi sita dhidi yako, kimekupa funzo gani?

SUGU: Nilichojifunza ni kwamba sasa Tanzania imeanza kuzalisha wafungwa wa kisiasa. Mimi nilifungwa kisiasa. Ukiniuliza nimepata funzo gani kama unavyoniuliza leo, ukweli kutoka moyoni mwangu, ooh kumbe Tanzania sasa imeanza kuzalisha wafungwa wa kisiasa.

SWALI: Changamoto kubwa inayolikabali Jimbo la Mbeya kwa sasa ni ipi na hatua zipi zimechukuliwa kuitatua?SUGU: Changamoto kubwa Mbeya Mjini kwa sasa ni baadhi ya viongozi wa CCM kutaka kuleta siasa uchwara kwenye masuala ya maendeleo tunayoyafanya pale chini ya mbunge ambaye ni wa Chadema na halmashauri ambayo pia iko chini ya Meya wa Chadema.

CCM wamekuwa wanafanya vitu ambavyo unaweza kuviita vya ovyo sana, ili kuvuruga mafanikio ya halmashauri iliyo chini ya Chadema na hata pengine kutaka ionekane kwamba mbunge hajafanya kitu chochote, lakini wananchi wa Mbeya si wajinga.

Pale kuna wasomi, wameelimika, wana ufahamu na wanamfuatilia mbunge wao na wanajua kila kinachoendelea.Kwa hiyo, tatizo la Mbeya Mjini ni siasa uchwara zinazoletwa kila siku. Lakini pia watendaji kama RC (Mkuu wa Mkoa), DC (Mkuu wa Wilaya) ambao wanaacha kutekeleza majukumu yao ya msingi, 'focus' yao inakuwa jinsi ya kumwangusha Sugu.

Mimi siangalii mtu mmoja mmoja, nakiangalia Chama Cha Mapinduzi kwa sababu hata mwaka 2015, kuelekea Uchaguzi Mkuu tulikuwa na kelele hizi hizi kuhusu dada yangu Mary Mwanjelwa. Mwanjelwa... Mwanjelwa... kelele zilipigwa kama sasa anavyotajwa Dk. Tulia (Ackson).

Lakini mwisho wake, sikugombea na Mwanjelwa, chama kilipitisha mtu mwingine kabisa tofauti. Kwa hiyo, nyinyi mnaozungumza pengine hamjui siasa za Mbeya na siasa za CCM wenyewe kule Mbeya.


Ziko tofauti sana. Pengine mnayemtaja kwenye mitandao na magazeti yetu, huenda asiwe yeye kwenye uchaguzi. Ndiyo maana mimi nasema mbele yangu siangalii mtu yeyote, mimi nakisubiri Chama Cha Mapinduzi.SWALI: Ni miaka mingi Sugu hajatoa wimbo mpya. Umeamua kuachana na muziki?

SUGU: Sijatoka kwenye muziki, kutokutoa wimbo hakuna maana kwamba nimetoka. Daktari asipotibu wagonjwa kwa siku mbili, tatu, haina maana kwamba ameacha udaktari.

Kwenye muziki bado tumo, lakini sasa hivi kutokana na 'situation', wewe ni mwanahabari unafahamu tumeshatoa mwongozo wa namna muziki wetu uwe.

Kwa sababu sasa tunaona ni vigumu kubaki, kuendelea kuwa 'professional artist', unaangalia sasa ni namna gani utaenenda.

SWALI: Ukiamka asubuhi na kujiangalia kwenye kioo, unaona nini mbele yako?

SUGU: Eeh... ninaiona 'future' yangu binafsi nikijaribu kuioanisha na 'future; ya taifa letu itakuwaje!

Na ninapovioanisha hivyo, ndiyo maana naacha kuwa 'selfish' (mbinafsi) katika mambo ya kitaifa, nayazungumza na kutoa mchango wangu na si tu kuangalia mimi kama mimi nimevaa suti nzuri, niko vizuri, basi niache kusema mambo ya msingi ya taifa.

Habari Kubwa