Sugu akamatwa akichukua fomu ya ubunge

15Aug 2020
Grace Mwakalinga
Mbeya
Nipashe
Sugu akamatwa akichukua fomu ya ubunge

MGOMBEA ubunge katika Jimbo la Mbeya Mjini kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Joseph Mbilinyi, na wanachama 15 wamekamatwa na polisi kwa tuhuma za kufanya maandamano kinyume cha sheria.

Majira ya saa 6:00 mchana, wafuasi wa CHADEMA pamoja na Mbilinyi, maarufu kama Sugu, walifika katika ofisi ya chama zilizoko Kata ya Sinde kwa lengo la kuanza pamoja safari ya kumsindikia katika ofisi za Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kuchukua fomu kuwania nafasi hiyo.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Ulrich Matei, alikiri Sugu na wenzake kukamatwa na kwamba lengo ni kupewa elimu juu ya mambo ya kuzingatia katika msimu huu wa kuelekea uchaguzi na kwamba wakati wa kufanya maandamano bado kwa sababu tume haijatoa majina na kibali cha kuanza kufanyika kwa kampeni, hivyo wangesubiri utaratibu.

“Nilipata taarifa kuwa Sugu leo (jana) anakwenda kuchukua fomu kwa maandamano makubwa ambayo yalianzia mitaa ya Sinde na wanachama hao waliamua kumsindikiza hadi ofisi za tume licha ya kutopewa kibali lakini pia kulikuwa na vurugu ambazo wanachama walizifanya walipofika katika ofisi za NEC,” alisema Matei.

Awali, akizungumza na waandishi wa habari wakati wa kukabidhiana fomu na kabla Sugu hajatiwa nguvuni, Msimamizi wa Uchaguzi ambaye pia ni Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Mbeya, Ademe Ng'wanidako, alisema alitimiza wajibu wake wa kumkabidhi fomu ili kwenda kuijaza na kutafuta wadhamini.

“Mimi kazi yangu tayari nimeitekeleza kwa kutoa fomu kwa mgombea. Kinachofuata akatafute wadhamini na kuzirejesha. Kuhusu kukamatwa kwa wafuasi wa chama hicho hizo ni habari nyingine,” alisema.

Katibu wa CHADEMA Mkoa wa Mbeya, George Tito, alisema kwa sasa wanashughulikia suala la dhamana na kujua sababu za kukamatwa kwa Sugu na wanachama wengine na kusisitiza kuwa maandamano ni kitu cha kawaida kwa kuwa wananchi ni wapigakura wake.

Tito alisema CHADEMA inalaani vikali kitengo kiichofanywa na Jeshi la Polisi kwa kuwa ni kuminya uhuru wa kidemokrasia katika kuelekea uchaguzi mkuu wa Oktoba 28, mwaka huu, kwa kuminya vyama upinzani na kufanya udhalilishaji wa hali ya juu.

“Kama chama tunaendelea kutafakari tukio hilo kwani kuna hujuma ambazo zinafanywa kukidhoofisha chama. Lakini tunasubiri uamuzi wa polisi kama kutakuwa na dhamana au la dhidi ya mgombea wetu ubunge na wanachama wetu 15,” alisema.

Habari Kubwa