Sugu asusa kusoma hotuba yake bungeni

19Apr 2019
Na Mwandishi Wetu
DODOMA
Nipashe
Sugu asusa kusoma hotuba yake bungeni

WAZIRI Kivuli katika Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Joseph Mbilinyi, maarufu Sugu, jana alisusa bungeni kusoma hotuba ya Kambi Rasmi ya Upinzani kutokana na uongozi wa Bunge kuagiza kufutwa kwa baadhi ya maneno yaliyoko kwenye kitabu cha hotuba hiyo.

WAZIRI Kivuli katika Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Joseph Mbilinyi.

Mara tu baada ya Sugu kuanza kusoma hotuba yake hiyo, Naibu Spika wa Bunge, Dk. Tulia Ackson, alimkatisha waziri kivuli huyo kusoma taarifa ambayo wanayo wabunge wengine, ambayo baadhi ya maneno yalikuwa yamefutwa.

Hata hivyo, Sugu alisema hawezi kusoma hotuba yake kwa kuwa anachotakiwa na uongozi wa Bunge kukisoma ndani ya Bunge siyo maoni yake bali maneno ya kulishwa.

Sugu alisema imekuwa kawaida ya Kiti cha Spika kuizuia hotuba yake kusomwa bungeni, akieleza kuwa hizo ni dalili za uoga wa serikali.

Kutokana na uamuzi huo wa Sugu kutosoma hotuba yake bungeni, Naibu Spika (Dk.

Ackson) aliagiza hotuba hiyo isiwekwe katika kumbukumbu za taarifa za Bunge.

 

Baadaye, akichangia mjadala wa hoja ya makadirio ya bajeti ya wizara hiyo, Sugu alisema pamoja na kuwapo kwa idadi kubwa ya vyombo vya habari nchini, bado hakuna uhuru wa habari. 

Sugu alisema Bunge pia limebariki hali hiyo kwa kuruhusu mijadala yake kutoonyeshwa moja kwa moja (live).

 

BAJETI UWANJA WA TAIFAMwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii, Peter Serukamba, alisema kamati yake imebaini bajeti ya kutekeleza miradi ya maendeleo ya wizara imepungua.

"Si hivyo tu, lakini pia mradi wa ujenzi eneo la Changamani la Michezo na hususan Uwanja wa Taifa na Uhuru haujatengewa fedha wakati mkataba baina ya nchi yetu na Jamhuri ya Watu wa China unafikia ukingoni mwezi Agosti 2019.

"Ikumbukwe kuwa wastani wa gharama za uendeshaji wa Uwanja wa Taifa na Uhuru ni takribani Sh. milioni 781 kwa mwaka," Serukamba alibainisha.

Alisema kamati yake inaishauri serikali kwa mara nyingine kuongeza bajeti ya maendeleo kwa wizara hiyo ili zipatikane fedha kwa ajili ya uendeshaji na ukarabati wa Uwanja wa Taifa na Uhuru.

Aliongeza kuwa kamati inaipongeza serikali kwa kuanzisha chaneli ya utalii (Tanzania Safari) kwa lengo la kuvutia watalii.

Habari Kubwa