Suleiman Kova kuagwa rasmi leo, TPS Moshi

22Jun 2016
Godfrey Mushi
Moshi
Nipashe
Suleiman Kova kuagwa rasmi leo, TPS Moshi

MKUU wa Jeshi la Polisi nchini, Ernest Mangu, leo anatarajiwa kuwahutubia askari, maofisa na makamishna wa jeshi hilo katika Shule Kuu ya Polisi Moshi (TPS), wakati wa sherehe ya kumuaga rasmi aliyekuwa Kamanda wa Polisi, Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Kamishna Suleiman Kova.

aliyekuwa Kamanda wa Polisi, Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Kamishna Suleiman Kova.

Taarifa iliyotolewa jana na Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP), Theresia Nyangasa, inaeleza kuwa IGP Mangu ataongozana na naibu wake, Abdurahman Kaniki.

Kwa mujibu wa Nyangasa, kabla ya IGP Mangu kutoa hotuba yake na kukabidhi zawadi, ataweka jiwe la msingi kituo cha afya cha shule hiyo ya polisi.

Mangu pia ataungana na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Yusuph Masauni, Juni 24, mwaka huu, katika sherehe za kufunga mafunzo ya awali ya Polisi na Uhamiaji yatakayofanyika kwenye viwanja vya paredi vya Shule ya Polisi-Moshi.

Kova aliyeiongoza Kanda Maalumu ya Dar es Salaam tangu Juni mwaka 2008, alistaafu Desemba, mwaka jana.

Kwa mara ya mwisho, Kova alizungumzia utumishi wake wa miaka 40 jeshini wakati wa hafla ya kuwatunuku vyeti vya utumishi bora askari na raia waliotoa ushirikiano kwa polisi, katika sherehe zilizofanyika viwanja vya Chuo cha Maofisa wa Polisi Kurasini, Desemba 31, mwaka jana.

Akizungumzia kustaafu kwake, Kova alisema katika kipindi alicholitumikia jeshi hilo hatasahau matukio matatu maishani mwake.

Alitaja matukio yanayoacha kumbukumbu ni uvamizi wa majambazi katika kituo cha Stakishari, kuanguka na Helkopta aliyokuwamo na aliyekuwa Makamu wa Rais, Dk. Ghalib Mohamed Bilal na aliyekuwa Waziri wa Ujenzi, Dk. John Magufuli.
Tukio la tatu ni mchakato wa Uchaguzi Mkuu uliopita.

Habari Kubwa