Suluhisho zimamoto

03Aug 2017
Christina Mwakangale
Dar es salaam
Nipashe
Suluhisho zimamoto

MAENEO yenye mkusanyiko mkubwa wa watu, ujenzi holela, ufinyu wa barabara, miundombinu hafifu na elimu duni ni kati ya sababu za kikosi cha Zimamoto kushindwa kufika kwa wakati katika matukio ya moto.

Aidha majiji makubwa ikiwamo Dar es Salaam, Mbeya, Arusha na Mwanza yanaongoza kwa matukio ya moto hususan katika makazi ya watu.

Kamishna Jenerali wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji nchini, Thobias Andengenye aliyasema hayo juzi jijini Dar es Salaam katika uzinduzi wa kampeni ya kuongeza ufahamu kuhusu majanga ya moto na matumizi ya namba ya dharura 114.

Aidha, kati ya watu 10, alisena Andengenye, ni wanne tu jijini wanaoifahamu namba ya dharura hivyo kampeni hiyo imelenga ifikapo 2020 asilimia 75 jamii iwe imefahamu kujiandaa na dharura ya moto.

Alisema changamoto iliyopo ni namna ya kufika kwenye matukio hayo haraka, kwa kuwa miji mikubwa ina maeneo mengi yenye makazi holela, barabara nyembamba zisizotoa nafasi ya magari kufika eneo la tukio.

Andengenye alisema kutokana na hali hiyo jeshi hilo limeanza mkakati wa kushirikiana na wakurugenzi wa halmashauri, miji, majiji ili ujenzi wa nyumba na makazi uzingatie kuacha nafasi iwapo tatizo linatokea.

"Mitaa ambayo iliachwa wazi kwa ajili ya kupita hivi sasa zimejengwa 'bar', maduka, vinyozi, 'grocery', hii inafanya kazi kuwa ngumu kufika kwenye tukio," alisema Andengenye.

Habari Kubwa