SUMAJKT yanunua magari, pikipiki kujiimarisha

04Aug 2020
Romana Mallya
Dar es Salaam
Nipashe
SUMAJKT yanunua magari, pikipiki kujiimarisha

SHIRIKA la Uzalishaji Mali la Jeshi la Kujenga Taifa (SUMAJKT), kupitia kampuni zake mbili SUMAJKT Guard na inayojishughulisha na usafi, zimezindua magari na pikipiki ya kujiimarisha kiutendaji.

Naibu Mkurugenzi wa Shirika la Uzalishaji Mali la Jeshi la Kujenga Taifa (SUMA-JKT) anayeshughulikia Utawala, Kanali Absolomoni Shausi, akikata utepe kuzindua magari na pikipiki zilizonunuliwa na kampuni zake za SUMA-JKT Guard na ya Usafi na Unyunyiziaji Dawa, katika hafla iliyofanyika jijini Dar es Salaam jana. Kushoto kwake ni Mkurugenzi Mwendeshaji wa kampuni hiyo, Luteni Kanali, Joseph Masanja. PICHA: ROMANA MALLYA

Vifaa hivyo, vinatokana na Sh. milioni 353.6 zilizotengwa na shirika hilo kuimarisha huduma ya vifaa kwa kampuni hizo.

Uzinduzi wa vifaa hivyo ulifanywa jana na Mwakilishi wa Mkuu wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), Brigedia Jenerali, Charles Mbunge ambaye ni Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa SUMAJKT anayeshughulikia Utawala, Kanali Absolomoni Shausi.

Brigedia Jenerali Mbunge alisema kupitia shirika hilo ametenga Sh. milioni 353.6 kwa lengo la kuimarisha kampuni hizo kivifaa.
“Vifaa hivi vinanunuliwa ili kuhakikisha miradi yote iliyopo chini ya shirika inapata vitendea kazi, kuongezeka kwa vitendea kazi kunaashiria ongezeko la wateja, malindo na ajira zimeongezeka,” alisema.

Aliwataka watendaji wanaosimamia miradi hiyo kuhakikisha vifaa hivyo vinatunzwa na madereva wahakikishe magari wanayokabidhiwa yanaleta faida na kukaa muda mrefu.

“Tunazihakikisha taasisi mbalimbali, sekta binafsi na watu binafsi ambao wanatumia huduma zetu kuwa tutaendelea kuzitoa kwa ubora zaidi na kwa wakati,” alisema.

Naye Luteni Kanali Joseph Masanja alisema mpaka sasa wana zaidi ya magari 40 na pikipiki zaidi ya 80 na hivi karibuni walinunua magari 11 kwa ajili ya usafi na ulinzi.

Alisema changamoto inayowakabili ni wateja kuchelewa kulipa ingawa jambo hilo serikali ilishalitolea maelekezo.

Alisema kampuni ya ulinzi wakati inaanza kazi mwaka 2010 baada ya usajili wake uliofanyika Oktoba 20, mwaka 2008, ilikuwa na walinzi saba, lakini kwa sasa wamefikia 11,214 na miongoni mwao wanawake ni 2,899.

Naye Meneja wa Kampuni ya usafi na unyunyiziaji dawa, Kapteni Rosemary Katani, alisema mradi umefanikiwa kununua magari mawili aina ya Canter ya tani 3.5 kwa Sh. milioni 55 na Tipper la tani 10 kwa Sh. milioni 103 kwa ajili ya kuzoa taka.

Alisema mradi umeajiri vibarua 448 wa kazi za usafi, umetengeneza sabuni kwa matumizi yao na wateja wa nje na kutengeneza vyungu vya kupandia maua.

Pia alisema kampuni ya usafi na unyunyiziaji dawa imeongeza washiriki kutoka 10 hadi 16 katika taasisi za serikali.

Habari Kubwa