Sumatra sasa kugawanywa

08Mar 2018
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Sumatra sasa kugawanywa

SERIKALI imesema inatarajia kuigawa Mamlaka ya Usafirishaji Majini na Nchi Kavu (Sumatra), ili kupata taasisi ambayo itashughulikia suala la usafiri wa majini.

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Prof. Makame Mbarawa.

Hayo yalibainishwa jana na Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Prof. Makame Mbarawa, alipokuwa akifungua Baraza la Wafanyakazi wa Mamlaka ya Hali ya Hewa, lililofanyika mjini hapa.

Alisema kugawanywa kwa Sumatra kutaiwezesha kupata kwa taasisi itakayoshughulika na usafiri wa majini na nyingine itajihusisha na nchi kavu.

Alisema kupatikana kwa taasisi hizo mbili kutawezesha TMA kupata fedha za tozo itakayoweka kwa huduma wanazotoa kwenye usafiri wa majini.

“Kuna fedha nyingi ambayo bado hatujaweza kuipata tulijaribu, lakini ilishindikana naamini safari hii itawezekana tunatarajia kuigawa Sumatra sasa tutaanzisha taasisi ambayo itasimamia mambo ya majini tu,”alisema.

Alisema baadhi ya mamlaka ambazo zinategemea TMA, zimekuwa zikitoa fedha kama tozo kwenye masuala ya hali ya hewa.“Kujenga imani kwa watu ni kazi kubwa sana na hii sasa kwa wananchi imeaminika, tuendeleze na kuisimamia kwa uadilifu ili Watanzania waendelee kutuamini,” alisema.

Akizungumzia ununuzi wa rada, Prof. Mbarawa alisema, Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA), itanunua rada nne zitakazo gharimu Sh. bilioni 63, kati ya fedha hizo asilimia 50 inategemea mapato ya ndani ya taasisi hiyo na zinazobaki zinatoka serikalini.