Sumaye awataka wanaCCM kuacha makundi

16Sep 2020
Na Mwandishi Wetu
Singida
Nipashe
Sumaye awataka wanaCCM kuacha makundi

WAZIRI Mkuu mstaafu, Fredrick Sumaye, amewataka wagombea wa nafasi za ubunge na udiwani kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), kuacha makundi ili kukisaidia chama kupata ushindi wa kishindo.

Sumaye aliyasema hayo jana alipokuwa akizindua kampeni za ubunge na udiwani, Jimbo la Singida Kaskazini, mkoani Singida zilizofanyika katika eneo la Kata ya Itaja.

"Mlikuwa wengi kwenye mchakato huu wa kuwania nafasi hizi, lakini sasa tumeshawapata wagombea hivyo tuwaunge mkono hao, nategemea kuwaona ninyi mliokosa nafasi hizi kushiriki kwenye kampeni ili kuwaunga mkono hao wagombea," alisema Sumaye.

Alisema kutokana na maendeleo makubwa yaliyofanywa na Dk. Magufuli chini ya CCM, wananchi wanapaswa kumchagua kuendelea kuwa rais na wabunge pamoja na madiwani wa chama hicho ili kukamilisha yote ya kimaendeleo aliyotarajia kuifanyia Tanzania.

Vile vile, Sumaye alisema Mwalimu Nyerere, aliikabidhi nchi kutoka mikononi mwa wazungu hivyo Watanzania hawatakuwa tayari kuwaachia wapinzania ambao hata kuongoza wilaya hawajawi na kuhoji kama wataweza kuiongoza nchi.

Aliwaambia wananchi wa jimbo hilo kama wanahitaji maendeleo wawachague wagombea wa CCM, akiwamo mbunge wa jimbo hilo, Ramadhan Ighondo na madiwani wake wote ili kumsaidia Magufuli kuleta maendeleo.

Aliwataka wananchi hao kumpa kura mgombea huyo ili akamalize mgogoro wa ardhi wa Kijiji cha Sagara, ambao wananchi wanadai fidia kutoka Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), huku akiwaahidi ndani ya miaka miwili umeme utakuwa umewaka kila kijiji katika tarafa ya Mgori ambayo ilitajwa kuwa na ukosefu wa umeme.

"Jamani nawaahidi mimi si napita hapa ndio njia yangu mnisimamishe ili mnizomee kama umeme hautakuwa umewaka katika hivi vijiji endapo mkimchagua Ighondo," alisema Sumaye.

Habari Kubwa