SUPA Breakfast ya EAST Africa Radio kuja kivingine

03Jun 2021
Christina Mwakangale
Dar es Salaam
Nipashe
SUPA Breakfast ya EAST Africa Radio kuja kivingine

KIPINDI cha redio cha SUPA Breakfast, kinachorushwa na East Africa, kinatarajia kuja na ubunifu mpya ambao utavutia wasikilizaji hususani vijana wa kisasa.

Watangazaji wapya wa kipindi cha SUPA Breakfast, kitakachorushwa na EA Radio kuanzia Jumatatu hadi Ijumaa, saa tatu asubuhi (kutoka kushoto), Chris Lugoe, Evans Bukuku na Bobby Mongi. PICHA: CHRISTINA MWAKANGALE

Chris Lugoe, Bobby Mongi na Evans Bukuku ni miongozi mwa watangazaji wapya ambao wataendesha kipindi hicho, kinachoanza saa tatu hadi saa nne asubuhi, siku za Jumatatu hadi Ijumaa.

Akizungumza na Nipashe mkoani Dar es Salaam, juzi, Lugoe alisema kutokana na uzoefu walio nao kwenye fani hiyo kwa takribani miaka 15, itakuwa chanzo cha kufanya kipindi kuwa bora zaidi kuliko awali.

“Umoja huu wa sisi watangazaji utafanya kipindi kuwa kizuri kuwakamata wasikilizaji zaidi hasa majira ya asubuhi ambayo kila mmoja anayesikiliza redio, atahitaji kufahamu kinachoendelea duniani,” alisema Lugoe.

Naye Bobby alisema kuwa uzoefu walio nao utaleta tofauti na kwamba pamoja na kukua kwa upatikanaji habari kupitia mitandao ya kijamii, bado wasikilizaji wa redio wana fursa ya kipekee kupata taarifa zilizohakikiwa.

“Tangu kipindi kinapoanza, tayari maandalizi yamefanyika vya kutosha, pamoja na mitandao ya kijamii kutoa taarifa, lakini redio tunatoa taarifa kamili, iliyothibitishwa na zenye usahihi,” alisema Bobby.

Pia Evans alisema kipindi hicho kilicho sheheni ubunifu mpya ikiwamo, burudani, taarifa za habari pamoja na mahojiano mbalimbali ndani ya studio, kitaanza Jumatatu ya wiki ijayo.

“Vipengele vipya kwenye kipindi hiki vitasaidia kudadavua ‘current issues’ ambazo zinatamalaki mitandaoni na sehemu zote katika vyanzo vya habari. SUPA Breakfast inamwanzishia msikilizaji siku pamoja na kumpa mwenendo wa nini kinaendelea nchini na duniani,” alisema Evans.

Kipindi cha SUPA Breakfast kina mchanganyiko wa matukio kadhaa, ikiwamo kufanya mazungumzo na wasilikizaji moja kwa moja, kupitia mitandao ya kijamii ya kipindi hicho na kwa njia ya simu.

Habari Kubwa