Taarifa mali za viongozi kielektroniki

11Mar 2017
Gwamaka Alipipi
Dar es Salaam
Nipashe
Taarifa mali za viongozi kielektroniki

KATIKA kuhakikisha viongozi wa umma wanaorodhesha taarifa zao sahihi za mali, Ofisi ya Rais, Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma imezindua mfumo wa kielektroniki wa menejimeti ya taarifa za kimaadili utakaowezesha kukusanya, kuchakata, na kutunza taarifa kwa urahisi.

Kamishna wa Sekretarieti hiyo, Jaji Mstaafu Harold Nsekela.

Chini ya mfumo huo, viongozi wa umma wametakiwa kuorodhesha mali zao pasipo kudanganya wala woga katika Sekretarieti ya Maadili ya Viogozi wa Umma.

Kamishna wa Sekretarieti hiyo, Jaji Mstaafu Harold Nsekela, aliyasema hayo jana jijini Dar es Salaam wakati wa uzinduzi wa mfumo huo ulioanza kujegwa Agosti, 2014 na kukamilika Novemba mwaka jana, ukifadhiriwa na Serikalio ya Canada kwa Dola za Marekani 33,040.

“Tukiwaita muitikie wito, taarifa mnazozitoa ni zenu wenyewe na mnapoleta taarifa za mali leteni taarifa za usahihi siyo za uongo, sisi tunasimamia maadili, hatukuchuguzi mali zako, tukikubaini tunakupeleka katika Baraza la Maadili tu,” alisema Jaji Nsekela.

Alisema walioshiriki kuanzisha mfumo huo ni Chuo cha Kompyuta cha Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam (UDSM), Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Wakala wa Serikali Mtandao, na Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma.

Alisema idadi ya watumishi wa umma ni 15,624, lakini viongozi wengi hawajafikiwa kuhakikiwa mali zao kutokana na ukosefu wa vitendea kazi na fedha.

Alisema kwa mwaka wa fedha 2016/17 kati ya watumishi 500 waliotakiwa kuhakikiwa mali zao, ni watumishi 116 tu waliofikiwa.
“Huu mfumo uliozinduliwa leo (jana) utarahisisha pia kuwafikia viongozi wengi na kuwahakiki mali zao,” alisema Jaji Nsekela.

Naye Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Utumishi wa Umma na Utawala Bora), Angellah Kairuki, alisema mfumo huo utarahisisha upatikanaji wa taarifa kwa wakati na ubora unaotakiwa.

Habari Kubwa