Taarifa ya DC yakataliwa CCM

06Dec 2019
Na Mwandishi Wetu
IGUNGA
Nipashe
Taarifa ya DC yakataliwa CCM

CHAMA cha Mapinduzi (CCM) wilayani Igunga mkoani Tabora kimekataa kupokea taarifa ya utekelezaji wa shughuli za serikali katika wilaya hiyo, kikieleza kuwa taarifa iliyowasilishwa imepitwa na wakati.

Mkuu wa Wilaya Tabora, John Mwaipopo.

Imedaiwa kuwa taarifa hiyo iliyowasilishwa juzi kwa Halmashauri Kuu ya chama hicho wilayani humo na Mkuu wa Wilaya hiyo, John Mwaipopo, ni ya Julai hadi Desemba mwaka jana badala ya Julai hadi Desemba mwaka huu.

Akitoa tamko hilo katika kikao hicho cha halmashauri kuu ya CCM wilaya, Mwenyekiti wa CCM wilayani humo, Regina Thadeo, alidai taarifa hiyo wamekataa kuipokea kwa imepitwa na wakati.

Alidai taarifa iliyowasilishwa katika kikao hicho cha ni ya utekelezaji wa shughuli za serikali kwa kipindi cha Julai hadi Desemba mwaka 2018 na sasa ni mwishoni mwa mwaka 2019,  hivyo hawawezi kuipokea na wanaona ni dharau kwa chama.

Aliongeza kuwa Halmashauri Kuu ya CCM wilaya ilimwelekeza mkuu wa wilaya huyo kuandaa upya taarifa ya utekelezaji wa shughuli za serikali katika wilaya hiyo.

Mkuu wa Wilaya ya Igunga, Mwaipopo, akizungumza na waandishi wa habari, alikiri kukataliwa kwa tarifa yake, lakini hakutaka kufafanua zaidi sababu za kupeleka taarifa iliyopitwa na wakati.

Habari Kubwa