Taasisi ya CCTTFA kusomesha watumishi wa MSCL

16Sep 2020
Neema Emmanuel
MWANZA
Nipashe
Taasisi ya CCTTFA kusomesha watumishi wa MSCL

Kampuni ya Huduma za Meli (MSCL) wametia saini ya makubaliano ya ufadhili wa kusomesha watumishi wa kampuni ya hiyo na Taasisi ya Kimataifa ya Kikanda ya CCTTFA.

Akizungumza leo wakati wa uwekaji saini ya makubaliano Ofisa Mtendaji Mkuu wa MSCL, Eric Hamissi amesema walianza mazungumzo tangu mwaka 2018 ili kuona uwezekanao wa taasisi hiyo kuwasaidia kujenga uwezo wa kiutendaji katika maeneo mbalimbali ambapo mazungumzo hayo yamezaa matunda baada ya CCTTFA kukubali kufadhili gharama za kusomesha watumishi wa MSCL ili kutekeleza majukumu yao kwa weledi na ufanisi zaidi.

Amesema makubaliano hayo yatadumu kwa kipindi cha miaka mitatu ambapo watumishi wa kada zote kuanzia Mabahari hadi Utawala wa MSCL watanufaika ambapo vyuo vinavyotarajia kutoa mafunzo hayo ni Chuo cha Bahari Dar es salaam (DMI),Chuo cha Usafirishaji cha Taifa (NIT) na Chuo cha Uzalishaji cha Taifa (NIP).

"CCTTFA ni taasisi ambayo inajishughulisha na kufanikisha usafirishaji wa mizigo inayopitia Ushoroba wa Kati  ikitokea Bandari ya Dar es salaam kuelekea nchi za jirani hivyo ufadhili ambao tumeweka saini una thamani ya million 209 na kwamba malipo yake yatafanyika moja kwa moja kwenda kwenye taasisi zitakazohusika na utoaji wa mafunzo hayo" anaeleza Hamissi.

Katibu Mtendaji wa Taasisi ya CCTTFA Kaptaini Dieudome Dukundane amesema lengo lao ni kuhakikisha biashara katika nchi tano washirika ambao ni Tanzania, Uganda, Rwanda, Burundi na DRC zinakuwa imara kwa kuangazia vifaa vya kusafirisha mzigo, ushindani wa kisiasa.

"Tunazo taasisi ambazo zinatoa ujuzi huo hivyo tumejiweka  tayari kuiunga mkono MSCL ili kushindana kibiashara " amesema Dukundane.

Naye Mkurugenzi wa Usafirishaji, Mazingira na Usalama, Stella Katondo akizungumza kwa niaba ya Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Dk Leonard Chamiriho amesema ni muhimu kuwa na wafanyakazi wenye ueledi watakosimamia na kuendesha kwa sababu vyombo hivyo vinabeba roho za watu lazima viwe salama hivyo Imani yao watakuwa na watumishi wenye ueledi watakaoitekeleza vyema nia ya Serikali.

"Nia ya Serikali na duniani kote lazima uwe na usafiri endelevu hivyo ni muhimu kuweza kutunza mazingira " ameeleza Katondo.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi MSCL, Prof.Zacheria Mganilwa ameeleza kuwa Serikali imeanza kuifanya nchi kuanza kutekeleza uchumi wa bluu kwa kuwajengea uwezo wafanyakazi , pia katika kipindi kifupi serikali imewekeza billion 153 kwenye kukarabati ujenzi wa meli mpya.

Ameongeza kuwa anaipongeza MSCL kwa kuaminika na kufanikiwa kupata kiasi hicho cha fedha ,pia anasema matarajio yao ni kuona meli zote zinaonekana majini zikiwa na ubora ili abiria anapotumia waweze kukudhi mahitaji yao na kupata starehe inayotakiwa na wafike kwa muda uliopagwa na mzigo yote ifike kwa ubora unaotarajiwa .

" Kwa ushirikiano huu lazima uchumi wa bluu utapanda watanzania tunawahakikishia tutasimamia vyema ili malengo yaweze kutumia tutatumia fursa ya uchumi wa bahari ya bluu kuendeleza maisha" ameeleza Mganilwa

Habari Kubwa