Taasisi ya Dk. Mengi yawatia watu wenye ulemavu moyo

20Jul 2019
Romana Mallya
Dar es Salaam
Nipashe
Taasisi ya Dk. Mengi yawatia watu wenye ulemavu moyo

MDHAMINI wa Taasisi ya Dk. Reginald Mengi iliyoanzishwa kwa ajili ya watu wenye ulemavu, ‘Dk. Reginald Mengi Persons with Disabilities Foundation,’ Jacqueline Mengi, amewatia moyo watu wenye ulemavu kwa kuwaeleza kuwa wataenzi mambo yote aliyoacha mwasisi wa taasisi hiyo.

Jacqueline Mengi.

Jacqueline aliyasema hayo jana jijini Dar es Salaam katika kongamano la kuwatangaza mabalozi wa tuzo za I CAN ambao ni miongoni mwa washindi walioshinda mwezi Machi mwaka huu.

Katika kongamano hilo, washindi hao ambao ni watu wenye ulemavu, walijadili na kutengeneza mkakati wa kuendeleza kazi na urithi wa Dk. Mengi aliyouacha katika taasisi hiyo baada ya kufariki Mei 2, mwaka huu.

“Nikiwa mdhamini wa taasisi hii na mjane wa Dk. Mengi, nawahakikishia watu wenye ulemavu, wafanyakazi na mkurugenzi wa taasisi hii, Shimimana Ntuyabaliwe, moja ya jambo muhimu ni kuendeleza yale aliyoacha,” alisema.

Jacqueline alimshukuru Rais John Magufuli; Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan; Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa; Spika wa Bunge, Job Ndugai; vyombo vya ulinzi na usalama na viongozi mbalimbali zikiwamo taasisi na mashirika kwa mchango wao wakati wote wa msiba wa Dk. Mengi.

“Kama familia hatuna cha kuwalipa, asanteni sana kwa sababu ukiwa na matatizo ndio utajua rafiki zako ni nani, kwa kweli Watanzania walionyesha kuwa ni marafiki wa Dk. Mengi,” alisema.

Pia alitoa pole kwa jamii ya watu wenye ulemavu kwa kuondokewa na baba, mlezi, mshauri na mtetezi wao.

“Ninajua sisi tumeondokewa, lakini nyie mmepata pigo kubwa sana, Dk. Mengi aliwapenda sana, haiwezi kupita siku au wiki bila kuzungumza marafiki zake, ndugu zake ambao ni watu wenye ulemavu, aliwapenda na kuwajali kwa dhati,” alisema.

Alisema Dk. Mengi alikuwa na ndoto ya kuona siku moja watu wenye ulemavu wakiondokana na changamoto za umasikini, kutothaminiwa, kunyanyaswa kubaguliwa na kutopewa heshima stahiki.

“Ameacha alama kubwa na funzo kwa jamii ya kutambua na kuheshimu watu wenye ulemavu na hiyo ndiyo heshima ya kipekee itakayodumu kwa miaka mingi ikimwakilisha Dk. Mengi,” alisema.

Alisema kutokana na ushauri alioutoa Waziri Mkuu, Majaliwa, wakati wa chakula cha mchana na watu wenye ulemavu miaka miwili iliyopita, alianzisha taasisi hiyo ya PWD.

Akizungumzia kitabu cha Dk. Mengi cha I Can, I Must, I Will, alisema kazi ya kukitafsiri kwa lugha ya Kiswahili alipewa Mhadhiri Mwandamizi wa Tafsiri na Taaluma za Kiswahili kutoka Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT), Dk. Hadija Jilala.

“Kazi ya kutafsiri kile kitabu chetu cha I Can, I Must, I Will, Dk. Mengi alimpa Dk. Jilala, kipo katika hatua ya mwisho ya kutafsiriwa, Dk. Jilala ni mmoja wa watu wenye ulemavu ambaye ni miongoni mwa mabalozi waliopewa nishani,” alisema.

Mkurugenzi wa Taasisi Mtendaji wa PWD, Shimimana, alisema matumaini yao ni kushirikiana na wadau wengine ili kujenga uwezo na kupanua wigo wa taasisi hiyo kuendesha kampeni na miradi mingi mikubwa kwa ajili ya kundi hilo.

Akitoa neno la shukrani, Dk. Jilala alisema kitendo cha kuitwa hapo na kupewa nishani kama mabalozi wa tuzo za I Can, inaonyesha wazi wapo na nia moja ya kuendeleza yale aliyoacha Dk. Mengi.

“Tunajivunia taasisi hii kama ni chombo pekee ambacho kinaweza kuweka alama kubwa ya Dk. Mengi, kama jamii ya watu wenye ulemavu tunatoa pole zetu kwa familia na kuwaahidi wewe ni mama yetu na sisi ni rafiki zako kama ambavyo tulivyokuwa kwa Dk. Mengi,” alisema.

Habari Kubwa