Taasisi ya Dk. Mengi yazindua tuzo kwa wenye ulemavu

07Dec 2018
Gwamaka Alipipi
Dar es Salaam
Nipashe
Taasisi ya Dk. Mengi yazindua tuzo kwa wenye ulemavu

TAASISI ya Dk. Reginald Mengi, inayojihusisha na watu wenye ulemavu (Dk. Reginald Mengi Persons with Disabilities Foundation), imezindua tuzo za ‘I CAN’ ili kuwaenzi na kuwahamasisha watu wenye ulemavu nchini wajione kuwa wanaweza.

Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Dk. Reginald Mengi Persons with Disabilities, Shimimana Ntuyabaliwe, akiwaonyesha waandishi wa habari nembo ya taasisi hiyo wakati wa kuzindua tuzo za I Can ambazo watazawadiwa watu wenye ulemavu, ili kuwaenzi na kuwahamasisha walemavu waliofanikiwa nyanja mbalimbali. Uzinduzi huo ulifanyika jijini Dar es Salaam jana. PICHA: SELEMANI MPOCHI

Tuzo hizo zitakazotolewa kuanzia mwakani zinalenga kuhamasisha mabadiliko ya kimtazamo kwa jamii ya watu wenye ulemavu ili waweze kujiamini kuwa wanaweza kufanya mambo makubwa sawa na wengine.

Mkurugenzi Mtendaji wa taasisi hiyo, Shimimana Ntuyabaliwe aliyasema hayo jana kwenye Makao Makuu ya IPP jijini Dar es Salaam na kueleza kuwa, lengo la tuzo hizo ni kuwabaini watu wenye ulemavu waliofanikiwa katika nyanja mbalimbali nchini ili kuwa mfano kwa jamii nzima.

“Madhumuni ya tuzo hizi ni kuhamasisha mabadiliko ya mtazamo wa jamii inayowazunguka watu wenye ulemavu, ili kuwaenzi na kutambua nafasi ya watu wenye ulemavu,” alisema Ntuyabaliwe.

Ntuyabaliwe alisema dhumuni lingine ni kuunga mkono Sheria ya watu wenye ulemavu ya mwaka 2010, haki ya kushiriki na kushirikishwa kikamilifu kwa watu wenye ulemavu katika mambo yote ya kijamii.

Alisema walengwa wa tuzo hizo ni Mtanzania yeyote mwenye ulemavu, ambaye kupitia uwezo alionao amepata mafanikio na ambaye safari yake ya maisha ni mfano mzuri wa kuigwa na watu wengine wenye ulemavu na jamii.

Ntuyabaliwe alivitaja vipengele vitakavyoshindaniwa kuwa ni pamoja na tuzo za mafanikio katika elimu, siasa, uongozi, ujasiriamali, sanaa na burudani, mafanikio katika michezo, tuzo ya kujitolea katika jamii pamoja na tuzo ya mafanikio katika ujuzi wa kipekee.

“Uteuzi wa tuzo hizi utazingatia namna shughuli husika imeleta ushawishi na msukumo wa mafanikio katika jamii, tutaangalia mafanikio, changamoto na vikwazo alivyopitia mhusika kufikia mafanikio husika,” alisema Ntuyabaliwe.

Alitaja masharti ya kushiriki tuzo hizo kuwa ni lazima mshiriki awe raia wa Tanzania mwenye kuendesha shughuli zake nchini, awe mlemavu wa aina yoyote na kwamba uteuzi utakaochelewa kuwasilishwa hautazingatiwa.

Alisema ili washiriki wa tuzo hizo waweze kupatikana, kwa yeyote anayemfahamu mtu mwenye vigezo hivyo anapaswa kupendekeza jina lake au aliye na ulemavu mwenyewe kujipendekeza kwa kuandika taarifa yake kisha kuiambatanisha na picha na baadaye kuituma katika ofisi za vituo vya utangazaji vya ITV/Redio One zilizopo maeneo mbalimbali nchini.

Alisema pia mshiriki anaweza kutuma taarifa hizo katika namba ya ‘Whatsapp’ ambayo ni 0692 141979 au barua pepe [email protected] na mwisho wa kutuma maombi hayo ni Januari 18, mwakani.

Alisema tuzo zitatolewa Februari 2, mwakani kwenye hafla ya chakula cha mchana itakayoandaliwa na Taasisi ya Dk. Reginald Mengi kwa ajili ya watu wenye ulemavu.

Alisema washindi watazawadiwa tuzo mbalimbali, cheti kitakachowekwa sahihi na Dk. Reginald Mengi na kupata nafasi ya kutambuliwa kitaifa pamoja na fedha taslimu.

Habari Kubwa