Taasisi yasaidia wanafunzi madaftari 10,998 Mwanza

20Jan 2022
Neema Emmanuel
MWANZA
Nipashe
Taasisi yasaidia wanafunzi madaftari 10,998 Mwanza

Taasisi ya The Desk & Chair Foundation, imetoa msaada wa madaftari 10,998 yenye thamani ya Shilingi milioni 10 kwa wanafunzi zaidi ya 700 wanaoishi kwenye mazingira hatarishi mkoani Mwanza.

Akizungumza baada ya kukabidhi msaada huo, Mwenyekiti wa taasisi hiyo, Alhaji Sibtain Meghjee, amesema taasisi yake imeamua kutoa msaad huo baada ya kuguswa na changamoto ya wazazi kushindwa kumudu gharama za kununua mahitaji ya shule kwa ajili ya watoto wao.

Amesema madaftari hayo yaliyotolewa kwa wanafunzi 720 wa shule za msingi na sekondari jijini Mwanza, yatasaidia familia zisizo na uwezo kwa kuwapunguzia gharama za mahitaji ya shule.

“Tunaipongeza serikali kwa jitihada za ujenzi wa madarasa na kutengeneza madawati kwa shule za sekondari,imewapunguzia wazazi mzigo wa kugharamia elimu hata wasio na uwezo watawapeleka watoto shule wasome,"amesema 

Amesema elimu ya uzazi wa mpango kwa wazazi ni muhimu  ili waweze kupanga idadi ya watoto ambao wataweza  kukidhi mahitaji yao.

Mbali na hayo ameishauri Wizara ya Elimu iangalie namna ya kuwapunguzia wazazi mzigo wa gharama za kununua sare,viatu na mahitaji mengine ya shule.

"Msimu wa shule zinapofunguliwa,vifaa vya shule kama sare,madaftari na viatu vyeusi huuzwa kwa gharama kubwa kulinganisha na viatu vya rangi nyingine kwa hali ilivyo  naishauri Wizara ya Elimu iwaruhusu wanafunzi  kuvaa mavazi ya nyumbani yenye heshima na viatu vya rangi tofauti,mfumo ambao unatumika nchini India ili kuhakikisha watoto wanakuwa shule badala ya mtaani,"amesema 

Amezishangaa baadhi ya shule za sekondari mwaka huu kuwaagiza watoto kwenda na leam mbili za karatasi badala ya moja,vifaa mbalimbali ikiwemo makwanja,mifagio,ndoo na majembe ambavyo hugharimu zaidi ya sh.200,000 kwa mtoto hivyo kuwawia vigumu wazazi wote kumudu gharama.

Taasisi hiyo imekuwa ikisaidia jamii katika masuala ya afya,elimu na maji mwaka jana ilitoa msaada wa madaftari yenye thamani ya sh. milioni 9,sare na viatu vya sh. milioni 3,misaada ambayo imetoa kwa miaka mitano na mwaka huu sare na viatu vitatolewa baada ya kupata fedha kutoka kwa wafadhili.

Baadhi ya wanafunzi walionufaika na msaada huo akiwemo Pendo Dorothei  amesema vifaa walivyowezeshwa vimewapunguzia wazazi gharama,vitawaongezea ari ya kujifunza kwa bidii na uandikaji wa notisi

Huku Emmy Benjamin,mwenye ndoto za udaktari wa binadamu akiahidi kufaulu vizuri mitihani yake ili kufikia malengo aliyojiwekea. 

Baadhi ya wazazi wa wanafunzi walionufaika na msaada huo Mariamu Nassoro, Madua Katumba na Prisca Lucas,kwa nyakati tofauti wameishukuru taasisi hiyo kwa namna inavyowasaidia watoto wa Watanzania masikini vifaa vya shule ili waweze kupata elimu na kuiomba taasisi hiyo iendelee kusaidia jamii yenye uhitaji.

Mbali na wanafunzi  hao pia vituo vya kulea watoto vya Kilema, Ihema,Tamsiya,Nitetee Foundation na taasisi ya Bilal Muslim Mission of Tanzania, Kanda ya Ziwa vilinufaika kwa msaada huo.

Habari Kubwa