Taasisi yataka mabadiliko sheria ndoa kulinda mtoto

16Jun 2021
Beatrice Shayo
DAR ES SALAAM
Nipashe
Taasisi yataka mabadiliko sheria ndoa kulinda mtoto

MKURUGENZI wa Sheria na Haki za Binadamu wa Taasisi ya Kujenga Jamii Jumuishi Tanzania (BISTO), Mussa Nzige, ameishauri serikali kurekebisha Sheria Ndoa ya Mwaka 1971 inayoruhusu mtoto chini ya miaka 18 kuolewa kwa ridhaa ya mzazi kama ilivyoamuliwa na Mahakama ya Rufani.

Nzige aliyasema hayo jana Dar es Salaam wakati akizungumza na waandishi wa habari katika kuelekea maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika ambayo hufanyika  Juni 16 kila mwaka.

Alisema kwenye kesi ya msingi namba 204 ya mwaka 2019 iliyoamuliwa na Mahakama ya Rufani kuwa kifungu cha 13 na 17 cha sheria hiyo kinapingana na Katiba ya Tanzania ya 1977 kwa kuweka umri tofauti wa kuoa au kuolewa kati ya mtoto wa kike na wa kiume.

Nzige alisema serikali inatakiwa kubadilisha sheria hiyo ambayo ina ubaguzi kwa watoto wa kike na wa kiume ndani ya mwaka mmoja mpaka sasa umekwisha na hakuna jitihada zozote zilizochukuliwa katika kutekeleza maamuzi ya mahakama.

Aidha, alisema Siku ya Mtoto wa Afrika, mashirika yasiyo ya kiserikali yamekuwa yakishirikiana na serikali katika kutoa elimu na kufanya ushawishi wa sera mbalimbali ili kuleta ustawi wa maendeleo ya taifa.

"Leo hii kituo cha kupinga ukatili wa kijinsia (CAGBV) kwa kushirikiana na Taasisi ya Bisto kwa pamoja katika kuadhimisha Siku ya Mtoto wa Afrika mwaka huu, na kuunga mkono uamuzi wa kitaifa na kimataifa imeona iangalie haki za watoto na hasa wale watoto wenye ulemavu hapa nchini," alisema.

Nzige alisema katika ajenda ya mwaka 2040 kundi la watoto wenye ulemavu bado limekuwa na mafanikio na changamoto zinazowafanya wasifurahie utoto wao kama watoto wengine.

Alisema kundi ambalo limekuwa likisahaulika bila kutajwa kwa upekee wake kama kundi maalum, hivyo jamii inatakiwa kuelewa Sheria ya Mtoto ya Mwaka 2009 ambayo ni msingi wa kutekeleza na kumlinda mtoto wanapotekeleza ajenda ya 2040.

Alisema watoto wenye ulemavu baadhi yao wamegeuzwa kitegauchumi na kunyimwa haki zao za msingi jambo ambalo halikubaliki.

"Kama una nguvu kwa nini usiende kufanya kazi na kumsaidia huyo mtoto badala ya kumgeuza kitega uchumi na kuzunguka naye kutwa ili ujipatie hela," alisema.

Aidha, alisema Tanzania ilipitisha sera ya maendeleo ya mtoto ya mwaka 2009 inayoelezea haki za mtoto. Mbali na nchi hizo imesaini mikataba mengine ya kimataifa kumlinda mtoto kama vile sheria ya utumikisha wa watoto katika vita, kwenye kazi na masuala ya kingono.

Habari Kubwa