Taasisi za fedha zajipanga kusaidia sekta ya kilimo

25Nov 2016
John Ngunge
ARUSHA
Nipashe
Taasisi za fedha zajipanga kusaidia sekta ya kilimo

TAASISI za fedha zimeshindwa kusaidia maendeleo ya kilimo kwa kutoa mikopo ya fedha, licha ya kukubaliana kufanya hivyo, kutokana na changamoto kadhaa zinazoikabili sekta hiyo.

Gavana wa Benki Kuu (BoT), Benno Ndulu.

Akitoa taarifa katika Mkutano wa 18 wa Taasisi za Fedha unaofanyika jijini hapa unaohusu namna Tanzania inavyopaswa kutumia fursa zake kuendelezaa nchi, Gavana wa Benki Kuu (BoT), Benno Ndulu, alisema, taasisi hizo zilishindwa kukidhi matakwa hayo.

Makubaliano ya kuongeza mikopo ya fedha kwa kilimo cha kibiashara, yalifikiwa kutokana na umuhimu wa sekta hiyo katika kupunguza umaskini, kutokana na wananchi wengi kujikita katika kilimo.

Kwa msingi huo, alisema BoT imetenga akiba yake kutoka asilimia 10 hadi asilimia nane, kwa lengo la kuweka ulinganifu kwa taasisi za fedha kutoa mikopo kwa sekta ya kilimo.

Profesa Ndulu, alisema azma ya kutoa mikopo kwa sekta ya kilimo ilikabiliana na changamoto miezi mitano baadaye ya mkutano huo kutokana na kudondoka kwa thamani ya shilingi miezi michache iliyopita.

Alisema kwa mfano, Machi 2014 na Machi 2015 thamani ya shilingi ilishuka dhidi ya dola kwa asilimia 9.6.

Alisema ili kuifanya shilingi iwe na thamani, BoT pamoja na juhudi zingine, imeamua kurejesha malengo ya kutoa mkopo kutoka asilimia 8 hadi 10.

Hata hivyo, Profesa Ndulu, alisema BoT itaendelea kuweka kanuni na mazingira mazuri yatakayosaidia kukua kwa taasisi za fedha ili ziweze kuchangia kukua kwa uchumi wa nchi.

Akifungua mkutano huo, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango, alisema taasisi za fedha bado hazijatumika kikamilifu kushawishi namna ya kutumia fursa zilizopo kwa maendeleo ya nchi.

Kuhusu ukosefu wa upatikanaji fedha, alisema ni suala linalokwamisha kukua kwa wafanyabiashara wadogo na wa kati.

Alisema upatikanaji wa fedha ni suala linalofungua kukua kwa fursa za kuzalisha ajira na kuchangia kukua kwa uchumi.

Alisema serikali imejidhatiti kupanua wigo na kuziwezesha taasisi za fedha kufanya biashara na kutoa huduma kwa jamii.

Habari Kubwa