Taasisi zajipanga kudhibiti mimea vamizi Ngorongoro

14Feb 2019
Na Mwandishi Wetu
Ngorongoro
Nipashe
Taasisi zajipanga kudhibiti mimea vamizi Ngorongoro

MAMLAKA ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA), imeanza kushirikiana na Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori (TAWIRI), Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA) na Kituo cha Utafiti wa Sayansi cha Nelson Mandela katika mkakati wa kutokomeza mimea vamizi katika bonde la Ngorongoro.

Mkakati huo umebainishwa na Mhifadhi Mkuu wa NCAA, Dk. Fred Manongi na kusema zaidi ya nusu la eneo la Bonde la Ngorongoro lenye ukubwa wa kilometa za mraba 250, limevamiwa na mimea hiyo ambayo siyo chakula cha wanyamapori.

Alisema SUA inaendelea na utafiti wa udongo ili kufahamu kiasi cha mbegu za mimea vamizi zilizomo katika udongo.

Aidha, alisema Taasisi ya Utafiti ya Nelson Mandela nayo inafanya utafiti wa kutumia aina fulani ya majani ya ukoka ambao umeonyesha mafanikio kwa asilimia 75.

Alisema ukoka huo unadhibiti mimea vamizi na kuangamiza mpaka mbegu zake, huku ukiruhusu kustawi kwa mmea mwingine unaofahamika kama Cynodon Dactylon, ambao ni chakula cha wanyamapori

Alisema taasisi hiyo ya utafiti imetenga maeneo matano maalumu ndani ya bonde la Ngorongoro na kuotesha huo ukoka, huku eneo moja likiwa nje ya bonde hilo sehemu ya Ndutu

“Mmea huu unavunwa na kusagwa na baadaye unalowekwa kwenye maji, unachuja na kunyunyuzia katika maeneo yaliyoathirika na mimea vamizi ambapo umeonyesha uwezo wa kudhibiti kwa asilimia 75 na uzuri wake ni chakula cha wanyama,”alifafanua.

Akizungumzia athari za mimea hiyo, Dk. Manongi alisema wanyamapori wanaokula majani wameanza kuhama maeneo yenye mimea hiyo na kwenda maeneo ya nje kutafuta majani mazuri

Alisema hali hiyo inatishia utalii kwa kuwa inawalazimu wanyamapori wanaokula nyama nao kuwafuata wale wanaokula majani nje ya bonde hilo

“Mimea hii vamizi huwa hailiwi na wanyamapori hivyo kuenea kwa kasi katika nyanda za malisho kutawafanya watoke nje kwenda kutafuta majani ambayo wanaweza kula na hivi hatua hiyo itafuatiwa na wanyama wanaokula nyama nao kuwafuta nje ya eneo,”alisema Dk Manongi

Kaimu mkuu wa idara ya usimamizi wa wanyamapori na nyanda za malisho katika mamlaka ya hifadhi hiyo na ambaye pia ni mwikolojia, Novatus Magoma, anasema wanaendelea kutumia njia za kuchoma moto na kung’oa mimea vamizi kwa kutumia timu za wenyeji kutoka vijiji vilivyomo ndani ya bonde hilo vya Oloirobi na Erkepusi na kwa mwaka jana aling’oa ekari 59.

Habari Kubwa